Madereva
wa vyombo mbali mbali vya moto nchini Tanzania, wanakusudia kushiriki
mgomo wa nchi nzima siku ya Ijumaa wiki hii, kuishinikiza serikali
kuondoa kero mbali mbali zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa ajira za
uhakika pamoja na agizo la kutaka madereva hao waende kusoma kila
wanapotaka kuhuisha leseni zao za udereva.
Wakizungumza
kupitia Katibu wa Muungano wa vyama vya Madereva Bw. Rashid Saleh,
madereva hao wamesema kuwa suala la kurudia
kusoma ni aina nyingine ya unyanyasaji kwa maelfu ya madereva nchini,
ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa hawana mfumo mzuri wa ajira licha
ya kutupiwa lawama kibao kuwa wao ndio chanzo cha ongezeko la ajali
nchini.
Katibu
huyo wa Muungano wa Vyama vya Madereva ameitaja kero nyingine kuwa ni
hatua ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT kutamka hadharani kuwa
vyeti walivyonavyo madereva hao sio halali na kwamba Ijumaa wiki hii
wanakusudia kukutana na Waziri wa Kazi na Ajira kwa ajili ya
kuzungumzia kero hizo kwa lengo la kuepusha kutokea kwa mgomo huo.