Kamanda wa Jeshi la Polisi Dodoma David Misime
Vikongwe watatu akiwemo mganga wa
kienyeji Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, wameuawa kwa tuhuma za kuzuia
mvua isinyeshe Wilayani humo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari na kamanda wa polisi mkoa wa Dodma, David Misime inasema kuwa
tukio la kwanza lilitokea Machi mosi mwaka huu majira ya saa saba
usiku katika kitongoji cha Golani, kijiji cha Masinyeti, kata ya
Iduo, tarafa ya Mlali.
Kamanda amesema katika tukio hilo mtu
mmoja aliyefahamika kwa jina la Saidia Chakutwanga (80) ambaye ni
mganga wa kienyeji aliuawa na watu waliojichukulia sheria mkononi
kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kutobolewa macho.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha
chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina wakimtuhumu marehemu
kuwa anazuia mvua kunyesha katika eneo hilo.
Katika tukio lingine amesema tarehe
hiyo hiyo majira ya saa nane usiku kwenye kitongoji cha Majengo,
kijiji cha Ihanda Kata na Tarafa ya Mlali mtu mmoja aliyemtaja kwa
jina la Peter Kaluli (85) akiwa na mkewe aitwaye Kaila Kaluli (80)
wakazi wa kitongoji cha Majengo wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao
ya tembe, waliuawa na watu wasiofahamika kwa kuangushiwa ukuta wa
nyumba yao kisha kuchoma moto na kubomoa nyumba mbili za tembe.
“Watu hao walifanya uharibifu
mwingine kwa kuwaua nguruwe mmoja na ng’ombe mmoja kumkata miguu
ambao ni mali za marehemu hao,” alisema Misime.
Kwa mujibu wa Kmanda uchunguzi wa awali
unaonyesha kuwa chanzo cha mauaji na uharibifu huo ni imani za
kishirikina wakiwatuhumu marehemu kuwa wanazuia mvua kunyesha.
Kutokana na tukio hilo watu wanne
akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihanda na wazee wawili wa kimila wa
kijiji wanashikiliwa na Polisi kuhusiana na tukio hilo kwani taarifa
zinaonyesha waliandaa vikao vya kutekeleza mauaji hayo.
Upelelezi wa matukio yote mawili
unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwatafuta watuhumiwa wengine
waliohusika na matukio haya ili sheri aiweze kuchukua mkondo wake.
Kufuatia tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Chiku Gallawa amewataka viongozi wa dini mkoani hapa kuhubiri
amani kwa waumini wao ili vitendo vya mauaji kwa vikongwe viweze
kukomeshwa.
0 comments:
Post a Comment