WAY

Thursday, November 20, 2014

HABARI ZA MTO ZA LEO ASUBUHI ZISOME HAPA


 SERIKALI YATOA TAMKO KUHUSU MALALAMIKO CHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
Serikali imetoa tamko kuhusiana na malalamiko ya Vyama vya siasa kuhusu kuingilia mamlaka ya vyama ya kuwapangia watu wa kuwadhamini Wananachama wao pamoja na Mihuri ambayo inatakiwa kutumika kutokana na Watendaji wa Vijiji kuwazuia wanachama hao kujiandikisha.

Akitoka Kauli ya Serikali jana Bungeni Mjini Dodoma Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda amesema Ofisi yake itatoa maelekezo kwa watendaji hao ili wananchama hao waweze kudhamini kutoka mashina au vitongoji vyao tofauti na ilivyokua awali.

Mh. Pinda ameongeza kuwa hatua ya Kufanya hivyo ni kutokana na migogoro iliyopo sasa ambayo inaonekana itaweza kuwanyima fursa wanachama wengine kushiriki katika chaguzi hizo na kusema hilo ni tatizo ambalo linarekebisha na wamefanya hivyo kwa maslahi ya Vyama vyote.

...................................
 WILAYA YA ROMBO YAONGOZA KWA UKATILI WA KIJINSIA
Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania inaogoza kwa ukatilia wa kijinsia na watoto huku ikibainika kuwa watoto ndio wamekuwa wahanga wa kubwa katika jamii.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa Kilimanjaro Bi. Grace Limo wakati wa Uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Duniani.

Bi. Grace amesema watoto wengi katika wilaya hiyo wanathirika kwa kutumikishwa katika shughuli za kibiashara na kwa kuachishwa shule huku wengine wakilelea na wazazi ambao wamejikita kwenye ulevi wa Kupindukia.

...................................
UKOSEFU ELIMU YA UZAZI SABABU YA MIMBA ZA UTOTONI SHINYANGA
Ukosefu wa  elimu ya uzazi na elimu ya uzazi wa mpango bado  ni changamoto  kubwa kwa wananchi wa halmashauri  ya  wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga,hali ambayo imekuwa ikisababisha kuongezeka kwa mimba za utotoni kwa kiasi kikubwa na hivyo kuhatarisha  maisha ya mama na mtoto.

Mratibu  msaidizi  wa huduma za afya  ya  uzazi na mtoto wa wilaya ya kishapu  Bi. Suzana Kulindwa ameyabainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema idadi  kubwa ya wasichana ambao wanabeba mimba kuanzia miaka 14 hadi 19.

Amesema kuwa kwa mwaka 2013 wanawake 13,373 walihudhuria kliniki na kati  yao 2,562  walikuwa na umri wa chini ya miaka 20 ikiwa ni sawa na asilimia 19.1 na kuwa  katika kipindi  cha  Januari na Juni mwaka huu wanawake 1,370  wenye umri wa chini ya miaka 20 walihudhuria Kliniki sawa na asilimia19.9 wakiwa wajawazito.

Amebainisha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2014, kati ya wanawake 6,871 waliohudhulia 1,370 , wamebainika ni vijana waliokuwa na umri wa chini ya miaka 20, hali aliyodai imekuwa ikisababisha kuwepo kwa ongezeko kubwa la vifo vitokanavyo na uzazi.
.....................................
MTU MMOJA AUWAWA NCHINI KENYA KATIKA MAPIGANO
Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mapigano katika mji wa Mombasa pwani ya Kenya.

Polisi walipambana na vijana walioingia katika Msikiti wa Swafaa eneo la Kisauni na mpaka sasa zaidi ya vijana 400 wanashikiliwa tangu kuanza kwa msako huo, mapema wiki hii.

Msako huo katika msikiti wa Swafaa mtaani Kisauni unakuja baada ya msako mwingine wa Jumatatu ambapo polisi pia walipata silaha ndani ya msikiti ambao wanasema hutumika kutoa mafunzo yenye itikadi kali.
................... .................
WANANCHI NCHINI MEXICO WAKUSANYIKA KUFANYA MAANDAMANO
Wananchi wa Mexico wamekuwa wakikusanyika kabla ya maandamano makubwa yaliyopangwa kufanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mexico City na miji mingine ili kupinga utekaji nyara wa wanafunzi arobaini na watatu.

Mikusanyiko mitatu ya maandamano itaungana katika lango la bustani kuu mjini Mexico City.

Shughuli za biashara na maduka katika eneo hilo yamefungwa kama njia ya kuchukua tahadhari huku Rais wa Mexico akisema nchi imeumizwa, lakini amani na haki ni mambo yanayotakiwa kusonga mbele
....................................
IRAQ YASEMA IMEKUBALIANA NA UTURUKI KATIKA VITA NA IS
Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi, amesema nchi yake na nchi jirani ya Uturuki, zimekubaliana kushirikiana kwa karibu kwenye masuala ya usalama na intelijensia, katika kukabiliana na kitisho cha kundi lijiitalo Dola la Kiislamu.

Haider ametoa kauli hiyo leo kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Baghdad, baada ya mazungumzo na mwenzake wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, aliye ziarani huko. 

Uhusiano kati ya pande hizo mbili ulikuwa mbaya kwa siku za hivi karibuni, kwa kile Iraq inachochukulia kuwa ni mauzo haramu ya mafuta yanayofanywa na jimbo la Kurdistan kupitia Uturuki.
................................
 TALGWU YAITAKA SERIKALI KULIPA MADENI YAKE
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) nchini, kimeitaka
serikali kuhakikisha inalipa madai ya wanachama wake yanayofikia kiasi
cha  shilingi bilioni 18 ,yanayotokana na malimbikizo ya mishahara
,uhamisho na masomo.

Akizungumza jana katika mkutano uliowakutanisha  viongozi mbalimbali  wa
TALGWU, Jijini Arusha, Mwenyekiti wa chama hicho,Seleiman Kikingo ametoa
tamko hilo, huku akisisitiza kuwa madai hayo yamedumu kwa zaidi ya
miaka mitano na serikali kupitia ofisi ya waziri mkuu ikiwa kimya.

Amesema pamoja na serikali kulipa kiasi cha shilingi bilioni 5,ikiwa
ni sehemu ya deni hilo jitihada zaidi zinahitajika kuhakikisha kuwa
madai yao yanakamilika kabla ya uchaguzi mkuu mwakani kufika,hatua
ambayo itawawezesha kujikimu na ukata unaowakabili.

Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo, amesisitiza kwa kuzitaka
halimashauri za miji na majiji hapa nchini kuunda mabaraza ya
wafanyakazi kwani katika halmashauri  167 za hapa nchini mabaraza
yaliyoundwa yapo 154 na kati ya hayo mabaraza 77 ndiyo yapo hai ,huku
mabaraza 73 hayapo hai.

MIGOGORO MINGI YA ARDHI NI UKOSEFU WA ELIMU YA ARDHI
Imebainika kuwa uwepo wa migogoro hiyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini licha ya kuchangiwa na utendaji mbovu wa viongozi wa serikali bado ukosefu wa elimu kwa wakulima umekuwa ni sababu ya wakulina na wafugaji  kushindwa kujua haki zao na hivyo kujikuta wakiingia katika migogoro ambayo ingeweza kumalizwa kwa misingi ya sheria.

Hayo yamebainika katika warsha ya wakulima na wafugaji wa mkoani Arusha chini ya Umoja wao wa MVIWATA na mtaalamu wa sheria wa  umoja huo Joseph Chiombola  na kuwataka viongozi mbalimbali wa siasa kutumia majukwaa yao katika kuwaelimisha wananchi ili kuepukana na migogoro iliyopo hivi sasa katika baadai ya maeneo.

Akifungua warsha hiyo  Mkuu wa wilaya ya Monduli Joika  Kasunga amesema migogoro ya ardhi ya mara kwa mara baina ya makundi ya wafugaji na wakulima yameifanya sekta hiyo kushindwa kuonyesha matokeo chanya,na hivyo kuwafanya kushindwa kufikia viwango vya kitaalamu katika uzalishaji wa mazao ya kilimo hali ambayo inatajwa kuwa kama itaendelea upo uwezekano wa usalama wa chakula nchini kuwa hatarini..

…............................................
 WANASHERIA AFRIKA MASHARIKI WAAZIMIA KUFANYA KAZI BILA MIPAKA
Wanasheria wa nchi wanachama wa Afrika Mashariki EAC, wamepitisha Azimio la kufanya kazi bila mipaka ndani ya eneo hilo lengo likiwa ni kupanua wigo wa kiutendaji kwa wataalalmu wa sheria walio katika eneo hilo.

Akizungumzia hatua hiyo, Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika mashariki EALS, aliemaliza Muda wake, James Mwamu, amesema azimio hilo litapitishwa na wanachama kabla ya kupelekwa mbele.

Kwa mujibu wa Mwamu, pendekezo la kuanzisha jambo hilo lilitoka kwa vyama vya wanasheria wanachama wa EALS kutoka Tanzania, Rwanda, Burundi, Zanzibar, Kenya, na Uganda.
…............................................
MEYA WA ASHKELON APINGA KUAJIRIWA WAARABU KATIKA MJI WAKE
Meya wa mji wa Ashkelon nchini Israel, Itamar Shimoni, amepiga marufuku kuajiriwa kwa Waarabu kwenye mji wake kwa kile anachokiita "sababu za kiusalama".

Akitangaza kupitia mtandao wake wa kijamii jana, meya huyo amesema wafanyakazi wa ujenzi ambao ni Waarabu wanaojenga mahandaki ya kujikinga na mabomu katika skuli za chekechea wanazuiwa mara moja hadi tangazo jengine litakapotolewa.

Wafanyakazi wengi wa ujenzi nchini Israel ni wa jamii ya Kiarabu, ambayo ni asilimia 20 ya raia wote wa nchi hiyo.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa serikali yake wameikosoa amri hiyo.

0 comments:

Post a Comment

.

.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...