Mashine ya kisasa ya kujiandikisha kitambulisho cha kura
Uandikishwaji wa Uboreshaji wa Daftari
la Kudumu la Wapiga kura Mkoani Njombe nchini Tanzania leo asubuhi
lilisimama kwa muda katika baadhi ya vituo kutokana na wananchi
kuzigomea mashine mpya zilizoongezwa kwa ajili ya Uandikishaji.
Akizungumza na East Africa Radio
msimamizi wa mashine za BVR, Astori Mgwame amesema kuwa wananchi hao
waligomea mashine hizo kwa kuwa zilikua hazina muendeshaji wa
kuziendesha kwa ufasaha na kusema kuwa hawatajiandikisha mpaka
wahakikishiwe kuwa kuna mtaalamu wa kuzitumia.
Mgwame ameongeza kuwa hali hiyo
inatokana na changamoto waliyokuwa nayo ya kuwa na upungufu wa wa
wataalamu wa kuziendesha mashine hizo hivyo kufanya zoezi kuenda
taratibu kushinda ilivyotarajiwa.
Aidha amesema changamoto nyingine
iliyojitokeza jana jioni mpaka kupelekea kufungwa kwa vituo hivyo
mapema kabla ya wakati ni kukatika kwa umeme na mashine kuishiwa
chaji na kuzima hivyo kushindwa kuendelea na zoezi hilo.
Mgwame amesema kuwa licha ya changamoto
hizo kujitokeza lakini uandikishwaji huo bado unaendelea vizuri na
wananchi wamejitokeza kwa wingi ili kuweza kupata haki yao hiyo ya
kujiandikisha.
0 comments:
Post a Comment