Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la
Yusufu Chatambala (45) mkazi wa Kijiji cha Makutupa Kata ya Lupeta
Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma, amehukumiwa kifungo cha maisha jela
baada ya kukiri kosa la kumbaka mtoto mdogo mwenye umri wa miaka
minne.
Mwendesha mashtaka wa polisi Godwill
Ikema ameiambia mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa kuwa mshtakiwa alitenda
kosa hilo Feb 20 mwaka huu majira ya saa 12 jioni katika kijiji cha
Makutupa kilichopo Wilayani Mpwapwa ambapo alimbaka mtoto mdogo wa
kike mwenye umri wa miaka minne
Mwendesha mashtaka huyo amesema kuwa
mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha sheria za nchi chini ya
Kifungu namba 130 (1) 2 (a) na 131 (1) cha Kanuni ya Adhabu kama
kilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002.
Amesema kuwa mshtakiwa alitenda kosa
hilo baada ya kumkamata alipokuwa akicheza na watoto wenzake jirani
na nyumbani kwao kisha kumpeleka kwenye shamba la mahindi kisha
kumbaka mtoto huyo na kusababishia majeraha na maumivu makali.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Wilaya ya Mpwapwa Paschal Mayumba alimtia hatiani mtuhumiwa huyo leo
baada ya kukiri kutenda kosa hilo.
Akisoma hukumu hiyo, hakimu Mayumba
amesema Mahakama inamhukumu kwenda jela kifungo cha maisha kwa kosa
la kubaka mtoto ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wanaotenda
makosa kama hayo.
0 comments:
Post a Comment