CHECK
AGAINST DELIVERY
HOTUBA
YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO
KIKWETE, AKIZUNGUMZA NA WAZEE WA MKOA WA DAR ES SALAAM,
TAREHE
22 DESEMBA, 2014
Shukrani
Mheshimiwa
Makamu wa Rais;
Mheshimiwa
Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Viongozi
wa CCM Mkoa;
Viongozi
Wenzangu;
Viongozi
wa Dini;
Wazee
Wangu;
Wananchi
Wenzangu;
Nawashukuru
sana wazee wangu wa Dar es Salaam, kwa kukubali mwaliko wangu na kuja
kuzungumza nami siku ya leo. Natambua kuwa taarifa ilikuwa ya muda
mfupi lakini mmeweza kuja kwa wingi kiasi hiki. Naomba radhi kwamba
ilikuwa tukutane Ijumaa lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu
tukaahirisha mpaka leo. Asanteni sana kwa uvumilivu wenu.
Kama
mjuavyo, kila ninapoomba kukutana nanyi ninalo jambo au mambo muhimu
kitaifa ambayo napenda kuzungumza nanyi, na, kwa kupitia kwenu taifa
zima linapata habari. Leo nina mambo mawili.
Wazee
Wangu;
Kwanza
kabisa, nataka kurudia kuwashukuru Watanzania wenzangu kwa moyo wenu
wa upendo mliouonyesha kwangu katika kipindi chote cha matibabu yangu
nikiwa nje na hata baada ya kurejea nchini. Kwa kweli nina deni kubwa
kwenu. Lazima nikiri kuwa, salamu zenu na taarifa kwamba watu
wamekuwa wananiombea uponaji wa haraka na uzima zinanipa faraja kubwa
na kunitia moyo. Nadhani zimechangia sana kuifanya afya yangu
kuendelea kuimarika kila kukicha. Bado sijawa “fit”
kabisa lakini naendelea vizuri. Hali yangu ilivyo sasa sivyo
ilivyokuwa wiki iliyopita au siku niliporejea nchini.
Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la kwanza ninalotaka kulizungumzia leo ni uchaguzi wa Serikali za
Mitaa uliofanyika Jumapili iliyopita tarehe 14 Desemba, 2014 na jana
tarehe 21 Desemba, 2014 katika maeneo ambayo uchaguzi huo
uliahirishwa. Bila ya shaka sote tumesikia taarifa ya awali ya zoezi
la upigaji kura iliyotolewa na Mheshimiwa Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tarehe 17 Desemba, 2014. Katika
taarifa yake hiyo, Mheshimiwa Waziri alieleza kwamba kwa jumla zoezi
limeenda vizuri kwenye maeneo mengi nchini. Uchaguzi ulifanyika kwa
ukamilifu katika Halmashauri 141
kati ya 162.
Katika Halmashauri 21 uchaguzi wake uliahirishwa na umefanyika jana
tarehe 21 Desemba, 2014.
Kwa
jumla, katika maeneo mengi uchaguzi ulifanyika kwa salama na amani na
hivyo kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowapenda
kuongoza vijiji vyao, vitongoji vyao na mitaa yao. Kufanyika kwa
uchaguzi huu ni uthibitisho mwingine wa kuendelea kukomaa kwa
demokrasia nchini. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati
kwa wale wote walioshiriki katika uchaguzi huu kwa maana ya vyama vya
siasa na wagombea. Natoa pongezi maalum kwa walioshinda. Nawaomba
sasa wakae chini kutengeneza mikakati na mipango ya kuwaongoza
wananchi wa maeneo yao katika kupata ufumbuzi wa changamoto za
maendeleo na za maisha, zinazowakabili.
Ndugu
wananchi;
Katika
taarifa yake hiyo pia, Waziri Hawa Ghasia alielezea masikitiko yake
kuhusu kasoro za uendeshaji wa zoezi zilizojitokeza katika maeneo
mbalimbali. Aidha, aliahidi kuchukua hatua stahiki za kinidhamu
dhidi ya watendaji na viongozi wa Serikali waliosababisha kasoro
hizo. Alifafanua kuwa miongoni mwa hatua zinazoweza kuchukuliwa ni
pamoja na kufukuzwa kazi, kusimamishwa kazi, kushushwa cheo, kukatwa
mshahara au kupewa onyo.
Napenda
kuelezea kufurahishwa kwangu na msimamo huo wa Waziri wa TAMISEMI na
nampongeza kwa hatua alizochukua. Namuunga mkono na namtaka aendelee
na msimamo huo katika kukabili vitendo vya utovu wa nidhamu wa
watumishi wa umma. Lazima kila mtumishi wa umma ajue kuwa
asipotimiza ipasavyo majukumu yake kuna adhabu inayolingana na kosa
alilofanya. Isitoshe, watu hao ndio watakaoendesha na kusimamia
Uchaguzi Mkuu wa mwakani wakiwa mawakala na wasaidizi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi. Hivyo basi, kuwajibishwa wale waliozembea katika
uchaguzi, itakuwa fundisho kwao na kwa wengine katika uchaguzi wa
mwaka 2015 na chaguzi nyingine zijazo.
Ndugu
wananchi;
Kwa
upande wa ghasia, fujo na ugomvi uliotokea wakati wa zoezi la
uchaguzi, nimezungumza na viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi na
kuwataka kuhakikisha kuwa wale wote waliofanya vitendo vya kuvunja
sheria wanatiwa nguvuni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Nimewataka wasifanye ajizi na watu wa aina hiyo. Hawa ni watu hatari
ambao hawana budi kuchukuliwa hatua thabiti za kuwadhibiti na
kuwaadabisha. Tusipofanya hivyo tunawakatisha tamaa raia wema na
watiifu wa sheria. Aidha, watu wakikamatwa na kuachiliwa muda mfupi
baadae, wakati mwingine hata bila dhamana ya namna yo yote
inawachanganya sana watu wema. Isitoshe tutakuwa tunalea maradhi ya
watu wabaya na kuwafanya waendelee kusumbua jamii. Nimewakumbusha
kuwa wasipokuwa wakali sasa tunaweka mazingira ya hatari ya kuja
kutokea mambo mabaya zaidi mwaka ujao kwenye uchaguzi mkuu.
Sakata
la Akaunti ya Tegeta ESCROW
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la pili ninalotaka kulizungumzia si geni masikioni kwenu, nalo ni
sakata la Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa
wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti mwezi Juni, 2014, kulitolewa
madai kuwa fedha zilizokuwemo katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta
iliyoko Benki Kuu zimechotwa kinyemela na mmiliki wa Kampuni ya Pan
African Power Solution (PAP) akishirikiana na Maafisa wa Serikali.
Serikali iliahidi
kufanya mambo mawili. Kwanza, kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa Akaunti hiyo na kwamba
taarifa yake itawasilishwa Bungeni. Na, pili, kumuagiza Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya
uchunguzi wa mwenendo mzima wa miamala katika Akaunti hiyo na kama
kuna uhalifu wo wote uliopo kwenye mamlaka yake achukue hatua
zipasazo kwa mujibu wa mamlaka na madaraka aliyonayo.
Ndugu
Wananchi;
Yote
mawili tuliyoahidi tumefanya. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali amefanya ukaguzi wa miamala katika Akaunti ya Escrow ya
Tegeta iliyoko Benki Kuu na taarifa yake ilishawasilishwa Bungeni.
Pia niliagiza taarifa hiyo ichapishwe kwenye magazeti na tovuti ya
Serikali ili watu waweze kuisoma. Agizo hilo nalo limetekelezwa.
TAKUKURU wameendelea na uchunguzi wao na watakapomaliza na kuridhika
kuhusu makosa yaliyofanywa watawafikisha wahusika Mahakamani.
Mkurugenzi Mkuu wa PCCB alifika kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali na kutoa baadhi ya mambo kuhusu suala hili
aliyoyaona ni muhimu Kamati iyajue.
Mambo
Manne Makuu
Ndugu
Wananchi;
Tarehe
8 Desemba, 2014 nilipoanza kazi baada ya mapumziko ya ugonjwa
nilikabidhiwa taarifa mbalimbali kuhusu sakata hili. Tangu wakati
huo nimekuwa nazisoma pamoja na kuzungumza na watu mbalimbali na
kuagiza nipatiwe ufafanuzi wa mambo mbalimbali kutoka kwa wahusika.
Shabaha yangu ni kuyaelewa vizuri mambo hayo ili niweze kufanya
uamuzi ulio sahihi na wa uhakika. Nimebaini kuwa yapo mambo makuu
manne:-
- Akaunti ya ESCROW
- Miliki ya PAP kwa IPTL
- Kodi za Serikali, na
- Tuhuma za Rushwa
Akaunti
ya ESCROW
Ndugu
Wananchi;
Katika
Mikataba ya Kununua Umeme (Power
Purchase Agreements)
ambayo TANESCO imetiliana sahihi na kampuni binafsi za kuzalisha
umeme za IPTL, SONGAS, SYMBION POWER na AGGRECO, kuna malipo ya namna
mbili yanayofanywa na TANESCO. Kwanza, hulipia umeme ilionunua
kutoka kwa kampuni hizo yaani tozo ya umeme (energy
charges).
Na, pili hulipia gharama za uwekezaji uliofanywa na kampuni hizo,
yaani tozo ya uwekezaji (capacity
charges).
Katika mikataba yote hiyo imekubaliwa kuwa iwapo kutatokea
kutofautiana, au mzozo unaohusu uwekezaji, upo utaratibu wa
usuluhishi. Utaratibu huo unataka kwanza kufanyike mazungumzo,
wakishindwa kuelewana watafute mtu wa kuwashauri na kuwasuluhisha;
wakishindwa kukubaliana wapeleke shauri lao kwenye Kituo (Mahakama)
cha Kimataifa cha Usuluhisi wa Migogoro ya Uwekezaji, (International
Centre for Settlement of Investment Disputes – ICSID) kilichopo
London, Uingereza
Ndugu
Wananchi;
Mwaka
1998 TANESCO walifikisha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa
Migogoro ya Uwekezaji, London, malalamiko kwamba gharama za uwekezaji
za IPTL ni kubwa mno kuliko kiasi halisi walichowekeza. Mwaka 2001
Kituo cha Usuluhisi kilifanya uamuzi wa shauri hilo. Madai ya
TANESCO yalikubaliwa kuwa uwekezaji halisi uliofanyika ni Dola
za Marekani 127
na siyo Dola
milioni 163.17 walizodai
IPTL. Kutokana na kupungua huko kwa gharama za uwekezaji, tozo ya
uwekezaji (capacity
charges)
nayo ilipunguzwa kutoka Dola
za Marekani milioni 3.6
kwa mwezi mpaka Dola
za Marekani milioni 2.6
kwa mwezi. Kituo pia, kilitoa mwongozo kuhusu ukokotoaji wa tozo
hiyo.
Ndugu
Wananchi;
Miaka
minne baadaye TANESCO ilianza vuguvugu la kutaka kupata nafuu zaidi.
Waliamua kugomea kulipa tozo ya uwekezaji kwa mkokotoo wa mwaka 2001.
Nimeambiwa kuwa wanasheria wa TANESCO walishauri Shirika hilo lidai
ukokotoaji kiwango cha tozo ya uwekezaji wa IPTL ufanyike kwa
kuzingatia thamani ya hisa walizolipia wawekezaji ambayo ni shilingi
50,000
badala ya kutumia msingi wa mtaji uliotokana na mkopo wa Dola
za Marekani milioni 38.16 wa wanahisa uliotumiwa na usuluhisho wa
kwanza ICSID-1.
Wakati
wakisubiri mchakato wa usuluhishi wa mzozo huu mpya kuanza, pande
zote mbili zilikubaliana kuanzisha Akaunti ya Escrow ya Tegeta.
Tarehe 5 Julai, 2006, akaunti hiyo ikaanzishwa kwa mkataba uliyotiwa
sahihi na IPTL upande mmoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba
ya TANESCO upande mwingine. Aidha, Benki Kuu iliteuliwa kuwa wakala
wa kutunza akaunti hiyo nayo ilitia sahihi.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
mujibu wa mkataba huo, Kampuni ya IPTL iliendelea kupeleka madai ya
tozo ya uwekezaji kwa TANESCO ambayo nayo iliwajibika kulipa madai
hayo. Malipo hayo yalitakiwa kupelekwa kwenye Akaunti ya Escrow ya
Tegeta tofauti na ilivyokuwa kabla ambapo yalipelekwa IPTL moja kwa
moja. Utaratibu huu mpya ulikubaliwa kutumika hadi pande mbili
zitakapofikia mwafaka kuhusu kiwango cha ukokotoaji. Kwa upande wa
malipo ya gharama ya umeme (energy
charges)
TANESCO imeendelea kulipa moja kwa moja kwa IPTL bila kupitia Akaunti
ya Tegeta ESCROW maana hizo hazikuwa na mgogoro.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
miaka saba tangu tarehe 5 Julai, 2006, akaunti hiyo ilipoanzishwa
mpaka tarehe 5 Septemba, 2013, wakati Mahakama Kuu ilipokabidhi
shughuli zote za IPTL kwa PAP, hakuna hatua stahiki zilizochukuliwa
kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa tozo ya uwekezaji baina ya ITPL na
TANESCO. Pande mbili husika hazikuwahi kukaa kuzungumza na wala
hakuna shauri lililofikishwa kwenye Kituo cha Kimataifa cha
Usuluhishi wa Mogogoro ya Uwekezaji kama ilivyofanyika mwaka 1998.
Wakati
wote huo, TANESCO iliendelea kulipa madai ya tozo ya uwekezaji ya
IPTL na kupeleka malipo hayo kwenye Akaunti ya Escrow. Ulipaji
ulisimama katika kipindi kifupi wakati kampuni ya IPTL ilipowekwa
kwenye ufilisi. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, wakati akaunti hiyo
inafungwa tarehe 20 Novemba, 2013, kulikuwa na fedha taslimu shilingi
8,020,522,330.37;
Hatifungani zenye thamani ya shilingi
159,231,370,000 na
Dola
za Marekani 22,198,544.
Fedha zote hizo ni sawa na shilingi
bilioni 202.9.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, kama TANESCO ingelipa tozo ya uwekezaji
ipasavyo, wakati huo Akaunti hii ingekuwa na shilingi
bilioni 306.7.
Kwa sababu ya kutolipa fedha zote ipasavyo, wakati Akaunti inafungwa
TANESCO walikuwa wanadaiwa na IPTL shilingi
bilioni 103.8.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Mauzo ya Umeme (PPA) malipo
yaliyocheleweshwa, yanatozwa riba ya
asilimia mbili
ya fedha zote ambazo hazikulipwa kwa wakati. Hivyo basi, riba
iliyotokana na TANESCO kuchelewesha malipo ilikuwa Dola
za Marekani
milioni
33.6.
Ni
matumaini yangu kuwa ufafanuzi uliotolewa katika Taarifa ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unasaidia kuweka kumbukumbu
sawa na sahihi kuhusu kiasi gani kilichokuwepo kwenye Akaunti ya
ESCROW siku uamuzi wa Mahakama ulipofanya akaunti hiyo ifungwe. Kwa
kifupi Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
inaeleza kuwa Akaunti hiyo ilikuwa na shilingi
bilioni 202.9
na siyo shilingi
bilioni 306.7
kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Fedha
za Nani
Ndugu
Wananchi;
Ni
matumaini yangu pia kwamba maelezo haya kwa kiasi fulani yamesaidia
kutoa jibu kwa swali maarufu la fedha za kwenye akaunti hii ni za
nani? Je ni za umma au za IPTL? Pengine nianze kwa kuelezea Akaunti
ya ESCROW ni nini? Akaunti ya ESCROW ni tofauti na akaunti nyingine
tunazozijua katika Benki zetu ambazo mtu anaweka fedha zake. Kama
tujuavyo, katika Benki zipo Akaunti za aina tatu ambazo wengi
tunazifahamu na kuzitumia yaani Akaunti ya Akiba (Savings Account),
Akaunti ya Hundi (Current Account) na Akaunti ya Muda Maalum (Fixed
Deposit Account). Akaunti ya Escrow ni akaunti maalum inayoanzishwa
kwa ajili ya kufanya kazi maalum, kwa masharti maalum na kazi hiyo
ikiisha akaunti yenyewe hufungwa. Akaunti hiyo husimamiwa na wakala
aliyeteuliwa kwa makubaliano ya wale wanaofungua akaunti hiyo.
Wakala ndiye mwenye jukumu la kusimamia akaunti na kumlipa mwenye
fedha wakati ukifika. Kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta pande mbili
husika zilikubaliana kuwa Benki Kuu ndiyo iwe Wakala. Ni muhimu
kujua kuwa akaunti hiyo ingeweza kufunguliwa kwenye Benki yoyote siyo
lazima BoT.
Akaunti
ya Tegeta ESCROW ilifunguliwa BoT mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi
fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity
charges)
zilizokuwa zinalipwa na TANESCO kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa
ambaye ni IPTL. Kabla ya hapo TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja
kwa IPTL. Kama nilivyokwishasema, awali ilifanyika hivyo ili kutoa
nafasi kwa pande hizo mbili husika kumaliza tofauti zao kuhusu
kiwango cha tozo ya uwekezaji ya IPTL.
Kimsingi
basi, fedha hizi ni za IPTL kwani ndiye mlipwaji na ni malipo
yanatokana na madai ya IPTL kwa TANESCO kuhusu tozo ya uwekezaji.
Hata hivyo, kwa mujibu wa CAG, inawezekana katika fedha hizo kuna
fedha za umma. Hi ni kwa namna mbili.
Kwanza,
kama mgogoro baina ya TANESCO na IPTL ungetatuliwa na kiwango cha
tozo ya uwekezaji kupungua kama ilivyofanyika mwaka 2001 katika
ICSID-1 na kama pande mbili husika zingekubaliana au kuagizwa kuwa
punguzo hilo lianze kuhesabiwa tangu tarehe ilipofunguliwa Akaunti
hiyo (tarehe 5 Julai, 2006), basi kungekuwepo pesa za kurejeshwa
TANESCO. Maadamu hili halikufanyika mpaka Mahakama ilipofanya
uamuzi uliosababisha akaunti hiyo kufungwa. Katika mazingira hayo
fedha zote zinakuwa ni za IPTL maana hakuna madai ya TANESCO.
Ndugu
Wananchi;
Namna
ya pili ni ile ambapo katika fedha hizi kunaweza kuwepo fedha za umma
na iwapo kuna kodi za Serikali ambazo hazijalipwa. Kwa mujibu wa
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na
kuthibitishwa na TRA ni kwamba kulikuwa na kodi ya VAT ambayo
haikulipwa. Nimeambiwa kuwa TANESCO ndiyo ilikuwa na wajibu wa
kukata kodi hizo kabla ya kulipa madai ya IPTL lakini kwa baadhi ya
malipo haikufanyika hivyo. Hivi IPTL inastahili kudaiwa kodi ya
Serikali? Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa, kodi inayotakiwa
kulipwa na IPTL ni shilingi
bilioni 21.7.
IPTL wameshapelekewa madai na TRA, na IPTL wamekubali kulipa.
Katika
ukaguzi wa Hesabu za TANESCO za mwaka 2012, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali aliwaelekeza TANESCO kuacha kuhesabu fedha
zilizopo kwenye Akaunti ya ESCROW kama ni fedha zao. CAG aliwaambia
TANESCO kwamba fedha hizo si zao.
Maagizo
hayo ya CAG yanasomeka kama ifuatavyo:
“As a result,
the deposit balance in Escrow account does not meet the definition of
an asset of the Company and therefore an adjustment has been made to
de-recognize the asset and related liability to the tune of the
amounts available in the Escrow account”
Kwa tafsiri
yake ni kuwa: “Hivyo basi, fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya
Escrow hazina sifa ya kutafsiriwa kama ni mali ya kampuni (TANESCO)
hivyo, marekebisho yamefanywa ili kutotambua mali na madeni
yanayohusu fedha hizo kwa kiasi cha fedha zilizopo kwenye akaunti ya
Escrow.”
Kutokana
na maelezo haya ni dhahiri kwamba, fedha zilizokuwa kwenye Escrow
siyo za TANESCO na hazikupaswa kuingizwa kwenye vitabu vya TANESCO
kama mali yake.
Chimbuko
la Sakata
Wazee
Wangu;
Chimbuko
la kadhia yote hii Bungeni na kwenye jamii ni uamuzi wa tarehe 5
Septemba, 2013, wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kuitambua PAP kuwa
mmiliki halali wa IPTL na kuagiza Mfilisi akabidhi shughuli zote za
IPTL kwa PAP. Katika utekelezaji wa uamuzi huo wa Mahakama Kuu
ukazuka mjadala mkali kuhusu fedha zilizomo kwenye akaunti ya ESCROW
kukabidhiwa kwa PAP. Kwanza kabisa mjadala ulikuwa ndani ya Serikali
miongoni mwa viongozi na watendaji wa Wizara na Taasisi zinazohusika
moja kwa moja na akaunti hiyo. Hizi ni Wizara ya Nishati na Madini,
TANESCO na Benki Kuu. Viongozi na Watendaji husika walikuwa
wanajiuliza na kuuliza kama walipe au wasilipe. Walipotaka ushauri
wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakaelekezwa watekeleze uamuzi wa
Mahakama Kuu. Alisema uko sawa na hauna matatizo. Halikadhalika,
Benki Kuu walipoulizia kuhusu kodi za Serikali, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali alielekeza kuwa hakuna kodi ya kulipwa.
Kwa
kuzingatia ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, malipo
yakafanyika kwa IPTL tena bila ya kodi kulipwa. Baada ya malipo
kufanywa ndipo mjadala huo ukahamia katika jamii na Bunge na kugeuka
kuwa kadhia kubwa iliyochukua sura ya kashfa yenye dalili za rushwa
na wizi.
Uamuzi
Unaotiliwa Shaka
Wazee
Wangu na Ndugu Wananchi;
Kwa
jumla uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu akaunti ya Escrow, ushauri wa
Mwanasheria Mkuu kwa Serikali wa kuelekeza uamuzi huo utekelezwe na
viongozi wa Serikali kutekeleza ushauri huo vimetiliwa shaka.
Umeonekana kuwa haukuwa uamuzi sahihi na kwamba umeitia hasara nchi.
Isitoshe uamuzi huo umeibua hisia za kuwepo harufu na vitendo vya
rushwa. Wapo waliosema si bure iko namna! Wapo waliotaja majina na
watu wanaodai wamepata mgao wa Escrow tena wengine wamechukua fedha
kwa viroba, sandarusi na rumbesa. Bahati mbaya sana katika mjadala
ilijengeka dhana isiyokuwa sahihi kwamba jambo hili lilianzishwa na
Maafisa hao wa Serikali kwa nia ya kujinufaisha wao binafsi. Ukweli
ni kwamba uamuzi ulifanywa na Mahakama Kuu na kwenye Serikali ilikuwa
utekelezaji wa amri hiyo.
Wazee
Wangu;
Nilipokutana
na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata maoni yake kuhusu
kadhia hii ameendelea kusema alichosema Bungeni kuwa hakukosea katika
ushauri wake na wala Mahakama haikufanya makosa. Hivyo basi, hakuona
sababu ya kwenda Mahakamani kuomba marekebisho ya uamuzi wa Mahakama
kuhusu fedha zilizokuwepo kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta
kukabidhiwa kampuni ya PAP mmiliki wa IPTL. Vilevile haoni kama kuna
hasara yo yote ambayo nchi imepata kwa sababu fedha zile ni za IPTL
na imelipwa IPTL.
Akifafanua,
alisema kuwa akaunti ya Escrow ilianzishwa kwa ajili ya kutunza fedha
za malipo ya tozo ya uwekezaji kwa IPTL yaliyokuwa yanafanywa na
TANESCO. Kabla ya mzozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo na kuanzishwa
kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta, TANESCO ilikuwa inalipa tozo ya
uwekezaji moja kwa moja kwa IPTL. Baada ya kutokea mzozo na akaunti
kuanzishwa mambo mawili hayakubadilika. Kwanza kwamba IPTL haikuacha
kupeleka madai ya tozo ya uwekezaji kwa TANESCO. Na, pili, kwamba
TANESCO haikuacha kulipa madai hayo. Mdai na mdaiwa hawakubadilika.
Kuwepo kwa akaunti ya Escrow hakubadili mwenye fedha zake. Akaunti
hiyo iliundwa kuhifadhi fedha za IPTL wakati suluhu inatafutwa kuhusu
kiwango cha tozo. Matumaini ni kwamba kama kiwango kitapunguzwa,
TANESCO inaweza kupata nafuu ya malipo.
Kuhusu
uamuzi wa Mahakama Kuu kuruhusu IPTL ilipwe fedha za akaunti ya
Escrow, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema ni uamuzi sahihi na wala
taifa halikupata hasara kwa sababu pesa zimelipwa IPTL na siyo mtu
mwingine. Isitoshe anaona uamuzi wa Mahakama umeisaidia TANESCO
kutua mzigo mkubwa iliyokuwa nao kwa miaka saba.
Kama
mjuavyo, akaunti ya Escrow ilianzishwa kuhifadhi pesa za malipo ya
tozo ya uwekezaji ya IPTL. Ilianzishwa kwa matumaini kuwa TANESCO
watapata nafuu ya tozo ya uwekezaji. Lakini, hapakuwahi kufanyika
mazungumzo baina ya TANESCO na IPTL kuhusu jambo hilo na wala suala
hilo halijafikishwa ICSID. Haikuweza kufanyika hivyo kwa sababu
washauri wa kisheria wa TANESCO hawajafanya hivyo. Wapo wanaodai
kuwa hawafanyi hivyo kwa sababu hakuna sababu mpya zinazoweza
kupatikana kuifanya ICSID ibadili uamuzi wake wa 2001 kuhusu kiasi
cha tozo na namna ya ukokotoaji wake.
Matokeo
yake ni TANESCO kuwa na akaunti ya Escrow ambayo mwisho wake
haujulikani. TANESCO inaendelea kudaiwa na IPTL tozo ya uwekezaji na
kulazimika kulipa kwenye akaunti hiyo. Kwa masharti ya akaunti ya
Escrow wanaposhindwa kulipa wanatozwa riba. Kwa mujibu wa taarifa ya
CAG mpaka tarehe 20 Novemba, 2013, TANESCO ilikuwa inadaiwa shilingi
bilioni 103.8
ambazo hawajalipa kwenye akaunti ya Escrow na riba ya Dola
za Marekani milioni 33.
Kwa sababu hiyo basi uamuzi wa kufunga Akaunti ya Tegeta Escrow
unalipatia unafuu TANESCO dhidi ya kulimbikiza madeni na riba.
Kwa
upande wa kodi za Serikali ambazo hazikulipwa, Mheshimiwa Jaji Werema
alisema yeye alitoa ushauri tu. Hata hivyo, kama mamlaka husika
inaona zipo kodi zinazostahili kulipwa izidai. Hakuna kilichopotea
kwa sababu anayedai, yaani TRA yupo, na mdaiwa yupo, IPTL.
Uamuzi
wa ICSID II Kuhusu Tozo ya Uwekezaji
Wazee
Wangu;
Yalitolewa
mawazo kuwa kama fedha za akaunti ya Tegeta Escrow zingelipwa baada
ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Kusuluhisha Migogoro ya
Uwekezaji (ICSID II) kutoa uamuzi wake, TANESCO ingepata nafuu ya
kupungua kwa tozo ya uwekezaji. Kuhusu jambo hilo nimeambiwa kwamba
kuna mambo mawili ya msingi. Kwanza kwamba Mahakama hiyo haikutoa
viwango vipya vya tozo kama ilivyofanya mwaka 2001 kwenye ICSID–I.
Haikubadili mwongozo wa ukokotoaji wa tozo. Imesema madai yanaweza
kuzungumzwa na kusisitiza kuwa katika mazungumzo hayo TANESCO
watambue kwamba wanahisa waliwekeza mtaji wao binafsi wakati wa
kununua mtambo na pia walikopa madeni, na kwamba kiasi cha fedha
walichowekeza kilitakiwa kiwe na kiwango cha juu zaidi cha faida.
Jambo
la pili ni kwamba, shauri hili la pili la ICSIDI II halikuihusisha
kampuni ya IPTL mwenye Mkataba wa Kuuza Umeme na TANESCO na siyo
Benki ya Standard Charterd. IPTL wameweka pingamizi la utekelezaji
wa uamuzi wa shauri hilo hapa nchini, hivyo inakuwa vigumu kwa
TANESCO kufanya mazungumzo kwa msingi wa shauri hilo.
Kinga
Dhidi ya Madai
Wakati
wa kufunga akaunti ya Escrow, upande wa Serikali ulielezea hofu yake
ya uwezekano wa siku za usoni mtu kudai tena kulipwa fedha hizi hizi
ilizolipwa PAP. Nimeambiwa kuwa suala hilo haliwezi kutokea kwani
limetengenezewa wigo imara wa kimkataba kuzuia. PAP imetiliana
sahihi na Serikali kwamba iwapo kutatokea mdai yo yote PAP
itawajibika kulipa.
Mashaka
ya Miliki ya PAP kwa IPTL
Ndugu
Wananchi;
Hofu
nyingine kuhusu uwezekano wa Serikali kupata hasara ni yale madai
kuwa huenda miliki ya PAP kwa asilimia 70 za hisa za IPTL zilizokuwa
za kampuni ya Mechmar Berhard ya Malaysia siyo halali. Pale mwanzoni
ilidaiwa kuwa kampuni ya Mechmar ilipouza hisa zake kwa kampuni ya
Piper Link ya British Virgin Islands ilikuwa chini ya mchakato wa
ufilisi kule Malaysia. Kama ingekuwa hivyo, kisheria mtu hawezi
kuuza hisa zake akiwa kwenye mazingira hayo. Katika uchunguzi wa CAG
alieleza kuwa amethibitisha kwamba madai hayo si kweli, Mechmar
walipouza hisa zao tarehe 9 Septemba, 2010 kampuni haikuwa kwenye
ufilisi. Iliingia kwenye mchakato wa ufilisi mwaka 2012.
Lakini
kwa upande wa kampuni ya Piper Link ya Uingereza inasemekana iliuza
hisa hizo baada ya kuwa wamepokea amri ya Mahakama ya Malkia ya BVI
kuizuia isiuze hisa hizo. Je ni kweli? Imefanyika hivyo? Kama ni
kweli je PAP waliponunua hisa hizo walijua kama kuna zuio au hapana?
Kama walijua basi na wao ni sehemu ya njama za kufanya udanganyifu.
Kama hawakuwa wamejua basi wametapeliwa. Nimeagiza uchunguzi wa kina
ufanyike kupata ukweli. Natambua hivi sasa Mahakamani zipo kesi
zinazohoji uhalali wa PAP kumiliki asilimia 70 za hisa za Mechmar
Berhad. Uchunguzi wetu hautaingilia mchakato huo lakini unaipa
Serikali fursa nzuri ya kuchukua hatua zipasazo kuhusu suala hili
lenye mjadala mkubwa. Jambo lingine muhimu ambalo limeleta matatizo
kwa Mahakama zetu nchini na BRELA ni uuzaji wa hisa za IPTL au
kuwekwa rehani hisa hizo bila ya uamuzi huo kusajiliwa BRELA na
kwenye Mahakama zetu. Sheria zetu ambazo ndizo za nchi ya Jumuiya
ya Madola kama ilivyo kwa Hong Kong, Malaysia, na BVI, inaitaka
kampuni ya Piper Link ya BVI iliponunua hisa za Mechmar katika IPTL
kusajili BRELA ununuzi huo. Hali kadhalika, inaitaka SCB ya Hong
Kong na kupata amri ya Mahakama kuzuia deni la Mechmar na kuwekwa
dhamana ya hisa za Mechmar katika IPTL. Piper Link isiuze hisa 70 za
Mechmar katika IPTL. Walitakiwa wasajili na BRELA na Mahakama yetu.
Kutokufanya hivyo ndiko kunazua maneno mengi na mzozo kuhusu uuzaji
wa hisa hizo kwa PAP. Kwa SCB wanapata usumbufu wa kudai madeni yao
IPTL kwa sababu hiyo hiyo. Uchunguzi utakaofanyika utapata ukweli wa
yote kwa uhakika.
Ndugu
Wananchi;
Taarifa
niliyopewa wakati najiandaa kuzungumza nanyi ni kuwa katika Mahakama
zetu nchini kuna mashauri yahusuyo miliki ya PAP ya hisa 70
zilizokuwa za Mechmar katika IPTL na yapo mashauri yahusuyo PAP
kupewa fedha za akaunti ya Escrow. Zipo pia nyingine za masuala
mbalimbali yakiwemo mashauri yaliyofunguliwa na PAP dhidi ya watu, na
makampuni binafsi na vyombo vya Serikali. Naamini uamuzi wa Mahakama
zetu utatoa majibu kwa masuala yote hayo.
Pamoja
na hayo yatakayokuwa yanaendelea Mahakamani, Serikali itaendelea
kufanya uchunguzi wake na kuamua namna ya kushughulikia taarifa
zitakazopatikana ili nayo iweze kwenda Mahakamani itakapolazimu
kufanya hivyo.
Jambo
lingine muhimu nataka uchunguzi wa kina ufanyike ni kujua nani ni
nani katika uuzaji na ununuzi wa hisa za Mechmar. Hususan nataka
tujue kwa ukweli na uhakika hisa hizo zimeuzwa kwa bei gani. Je, ni
kweli gharama zinazosemwa ndizo zenyewe? Nataka kuthibitisha ukweli
huo ili tujue kodi yetu ya ongezeko la mtaji (Capital
Gains Tax)
inayostahili kulipwa Tanzania ni kiasi gani? Je kiasi gani kimelipwa
na kipi hakijalipwa ili kidaiwe?
Tuhuma
za Kuwepo kwa Harufu ya Rushwa
Wazee
Wangu;
Kumekuwepo
na tuhuma za vitendo vya rushwa katika mchakato mzima wa kufunga
akaunti ya Escrow na kukabidhi fedha hizo kwa kampuni ya PAP.
Halikadhalika, kumekuwepo na hisia hizo hizo kwa upande wa jinsi
kampuni ya VIP Engineering and Marketing ilivyotumia pesa zake
zilizoko kwenye Benki ya Mkombozi. Yamesemwa mengi sana na
mmeyasikia na kuyasoma.
Rushwa
ni kosa la kijinai ambalo kwa Serikali yetu ni kosa ambalo ni vigumu
kulivumilia wala kulifumbia macho. Mara baada ya kupata fununu za
uwezekano wa vitendo hivyo kufuatia taarifa ya awali ya CAG ya kwenda
kukagua miamala, niliagiza taarifa husika zifikishwe kwenye Taasisi
ya Kupamba na Kuzuia Rushwa (PCCB) kwa uchunguzi zaidi. Naambiwa
taarifa hizo zimefika na kazi ya uchunguzi inaendelea. Tayari watu
kadhaa wamehojiwa na wengine wanaendelea kuhojiwa. Wakati nawasihi
wananchi kuvuta subira ili tuwape nafasi PCCB wakamilishe kwa ufanisi
wa hali ya juu kazi yao waliyokwishaianza, nawaomba PCCB waongeze
kasi ya uchunguzi. Napenda kufafanua kwamba kwa upande wa miamala
iliyotoka katika akaunti ya kampuni ya VIP Engineering and Marketing
ya Ndugu James Rugemalila, Serikali inashughulika na watumishi wa
umma kwa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma, maana
suala lao ni la kimaadili. Hatuwahoji wasiokuwa watumishi wa umma.
Maazimio
ya Bunge
Ndugu
Viongozi;
Wazee
Wangu;
Ndugu
Wananchi;
Niliona
nianze kwa kutoa maelezo hayo ya utangulizi kabla ya kuyazungumzia
maazimio ya Bunge. Serikali imepokea maazimio hayo ya Bunge na
kuyafanyia kazi kwa ajili ya utekelezaji wake. Nawapongeza Wabunge
wetu kwa moyo waliouonesha wa kuchukia maovu na kutaka yashughulikiwe
ipasavyo. Napenda kuwahakikishia kuwa niko pamoja nao. Nampongeza
Mheshimiwa Anna Makinda, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu
Spika na Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Mussa Zungu kwa uongozi wao
mahiri. Hakika haikuwa kazi rahisi, lakini chini ya uongozi wao
mambo yameisha salama na tumepata maazimio nane
yanayozungumzika
na kutekelezeka. Nawashukuru na kuwapongeza sana Wajumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya uongozi wa
Mheshimiwa Zitto Kabwe na Mheshimiwa Deo Filikunjombe na pia Wajumbe
waliounda Kamati ya Mapendekezo kwa kufikia mwafaka wa mapendekezo
haya 8 ambayo yaliazimiwa na Bunge.
Mwisho
lakini si ya mwisho kwa umuhimu, nawapongeza Wabunge wote kwa
michango yao mizuri. Jambo lililonifurahisha sana ni ushirikiano wa
Wabunge wa kambi zote katika kutafuta ufumbuzi wa suala hili muhimu,.
Hivi ndivyo inavyotakiwa Bunge liwe. Kwa kweli lazima nieleze
mshangao wangu niliposikia kambi ya upinzani ikijaribu kufanya
maamuzi yale ni yao wao na wenzao hawamo. Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali ina Wajumbe 19
wa CCM na wa Upinzani 5.
Bunge lina Wabunge wa CCM asilimia
74 na
wa upinzani asilimia
26.
Hivi kama ni yao wao pekee na wa upande wa CCM wangepinga yangekuwa?
Yasingefika po pote, yangefia kwenye Kamati. Huku ni kutafuta
umaarufu kwa mgongo wa wengine. Na, Wabunge wengi wa CCM na nyie
semeni msikike kwa uamuzi mliyofanya wote.
Napenda kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini hatuna
upungufu wa dhamira ya kutekeleza yale maazimio yanayoangukia katika
dhamana yetu. Napenda kuainisha mtazamo na mwelekeo wa Serikali
katika utekelezaji wa maazimio hayo manane
kama ifuatavyo:-
Azimio la
kwanza:
Serikali iangalie uwezekano wa kuchukua mitambo ya kufua umeme ya
IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Pendekezo
tumelipokea, ni jambo linalowezekana kufanya. Hata hivyo, tunapopima
ujumbe tunaoupeleka kwa jumuiya ya wawekezaji tunachelea kuwa inaweza
kuleta hofu na kuwatisha wawekezaji waliopo na wajao. Nalisema
hivyo kwa sababu sisi tuna historia ya kutaifisha mali za kamapuni
binafsi. Hofu hiyo bado ipo. Tukichukua mitambo hii tunaweza
kurudisha hofu za kurudi tulikokuwa na kukimbiza mitaji tunayohitaji
kwa uchumi kukua na nchi kupata maendeleo. Nashauri tuendelee
kuyapatia ufumbuzi matatizo ya IPTL kila tunapoyabaini. Aidha,
Mahakama imetusaidia sana kwa kuamuru mitambo ya IPTL ibadilishwe ili
itumie gesi asilia na kutoza bei ya umeme isiyozidi senti
nane za Marekani.
Tuyafuatiliye haya kwanza.
Azimio la
Pili:
Azimio hilo linazungumzia kuhusu uwazi wa Mikataba linasomeka
ifuatavyo: “Bunge limeazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio
husika la Bunge mapema iwezekavyo na kwa vyovyote vile kabla ya
kumalizika kwa Bunge la Bajeti. Serikali iwasilishe taarifa ya
utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme”.
Azimio
hili tumelipokea na tunaangalia namna bora ya kulitekeleza ili kuweza
kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza, kuitikia kilio cha muda
mrefu kuhusu uwazi katika mikataba ambayo Serikali inaingia na
wawekezaji; na pili kuhakikisha usiri wa mikataba hiyo ambayo ni haki
ya wawekezaji hao dhidi ya washindani wao inazingatiwa. Serikali na
Bunge tutakaa chini hivi punde kutafuta namna bora ya kisheria na
tutafanya hivyo kwa kujifunza pia kutokana na uzoefu wa nchi ambazo
zina utaratibu wa aina hii.
Azimio la
Tatu:
Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba TAKUKURU, Jeshi la Polisi na
vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahili
kwa mujibu wa sheria za nchi yetu dhidi ya watu waliotajwa kwenye
taarifa maalum ya Kamati husika na vitendo vyote vya kijinai
kuhusiana na miamala ya Akaunti ya ESCROW, na watu wengine
watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusu
kuhusika kwao katika vitendo hivyo vya jinai”
Vyombo husika vimekwishaagizwa kufanya hivyo na kazi imeanza na
inaendelea. Ikiwa wapo watu wenye makosa hatua zitachukuliwa kwa
mujibu wa sheria.
Azimio la
nne:
Linasomeka, “Kamati za Bunge kuwavua nyadhifa zao wenyeviti wa
Kamati za Bunge waliotajwa kupewa fedha na kampuni ya VIP Engineering
kabla ya kikao kijacho cha Bunge”
Azimio
hilo liko chini ya mamlaka ya Bunge lenyewe. Nawaachia wao waamue.
Azimio la
Tano:
Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza utovu wa
maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes
Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania”
Azimio
hili nimelipokea, tumelijadili hata hivyo, itabidi tufuate utaratibu
wa kikatiba na kisheria wa kushughulikia masuala ya namna hiyo.
Inatakiwa suala kama hili lianzie kwenye Mhimili wa Mahakama yenyewe
na siyo kwa Rais au Bunge. Tume ya Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya
kumtaka Rais aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji yeyote
pale inaporidhika kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo.
Nashauri suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie
atakavyoona inafaa.
Azimio la
Sita:
“Bunge linaazimia kwamba mamlaka husika za kifedha na za
kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Ltd. na benki yeyote
itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka ya uchunguzi,
kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya
ESCROW kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu
(Institutions of money laundering concerns).
Pendekezo
la Bunge ni zuri kwamba mamlaka husika na udhibiti wa vitendo vya
utakatishaji fedha vifanye uchunguzi kwa mujibu wa Sheria. Serikali
imelipokea na mamlaka husika yaani Financial Intelligence Units
kulishughulikia. Naamini wameshaaza, tuwape muda watimize wajibu wao
kwa mujibu wa sheria.
Azimio la
Saba:
“Bunge liliazimia kwamba Serikali iandae, na kuwasilisha Muswada
wa Marekebisho ya Sheria iliyounda TAKUKURU kwa lengo la kuanzishwa
Taasisi mahsusi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo vya
rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa
kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kazi
ya kufanya mageuzi katika TAKUKURU inaendelea. Tayari Sheria
mbalimbali zimetungwa ikiwa ni pamoja na Sheria Mpya ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa ya mwaka 2008, Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya
Fedha Haramu ya mwaka 1991 ambazo zote zinaweka utaratibu wa
kushughulikia vitendo vya rushwa. Tutaendelea kuziboresha sheria
hizo kwa kadri itakavyohitajika. Kazi iliyopo mbele yetu ni
kuimarisha usimamizi wa sheria hizo. Jambo hilo nalo litazingatiwa
katika maboresho hayo. Ni dhamira yangu na ya Serikali ninayoiongoza
kupambana na kushinda vita dhidi ya rushwa. Kwa hiyo tuko tayari
kulifanyia kazi pendekezo lolote linaloimarisha dhamira yetu hii
njema.
Azimio la
nane:
“Bunge linaazimia kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa
Ardhi na Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi ya TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi
kutengua uteuzi wao.
Azimio
hili ndilo Azimio ambalo limevuta hisia za watu wengi, na pengine
ndilo ambalo utekelezaji wake unasubiriwa kwa hamu. Utekeelzaji wake
umeanza. Kwanza, ni kuhusu Bodi ya TANESCO, tumeanza mchakato wa
kuunda Bodi mpya kwani iliyopo imemaliza muda wake. Kuhusu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni mtumishi wa umma
anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa umma, hivyo
nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika
ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa. Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ameshajiuzulu. Tumelitafakari suala la Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi la kupokea fedha kutoka VIP Engineering
and Marketing ambazo kwa maelezo yake ni kwa ajili ya shule
anayoimiliki na kuiendesha. Mwenyewe ameeleza wazi kupitia vyombo
vya habari. Pamoja na hayo yapo mambo ya msingi kimaadili ambayo
hayakuzingatiwa, hivyo tumemwomba atupishe tuteue mwingine. Kuhusu
Prof. Muhongo nimemuweka kiporo, kuna uchunguzi niliagiza ufanywe na
vyombo vyetu bado nasubiri taarifa hiyo ili nifanye uamuzi ndani ya
siku chache zijazo.
Hitimisho
Wazee
Wangu;
Nawashukuruni
kwa kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment