Mwanasheria mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema akiwa na Mbunge David Kafulila
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya
Tanzania, Jaji Frederick Werema amejiuzulu nafasi yake hiyo kuanzia
jana, Jumanne, kufuatia sakata la uchotaji wa fedha kutoka akaunti ya
ESCROW ambapo zaidi ya Sh. Bilioni 320 zilihamishwa.
Mwanasheria mkuu, pamoja na baadhi ya
wanasiasa na maafisa waandamizi wa serikali walituhumiwa kuhusika kwa
namna moja au nyingine kufanikisha kufanyika kwa miamala haramu ya
fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, Dar es Salaam, imesema Rais Jakaya Kikwete amekubali ombi hilo
la kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali.
Katika barua yake kwa Rais Kikwete,
Jaji Werema amesema ameomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake
kuhusiana na suala ya Akaunti ya Tegeta Escrow haukueleweka na
umechafua hali ya hewa. Rais Kikwete amemshukuru Jaji Werema kwa
utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na uadilifu.
Sakata la Akaunti ya Escrow liliibuliwa
bungeni na mmoja wa wabunge wa bunge la Tanzania, David Kafulila na
kusababisha mjadala mkali na kuamua Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali kupewa jukumu la kuchunguza kashfa hiyo.
Baada ya uchunguzi kuwasilishwa katika
mkutano wa bunge uliomalizika mwishoni mwa mwezi Novemba, kamati hiyo
ilikuja na maazimio manane kuhusu taarifa ya ukaguzi maalum kuhusiana
na miamala iliyofanyika katika akaunti ya Escrow ya Tegeta pamoja na
umiliki wa kampuni ya IPTL.
Miongoni mwa maazimio ya bunge
yaliwataja baadhi ya wanasiasa, mwanasheria mkuu, maafisa waandamizi
wa serikali, majaji, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini,
mawakili wa kujitegemea na watu binafsi kuhusika katika kashfa hii na
hivyo kuagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua za kisheria
wahusika na wengine kuondolewa katika nyadhifa zao za kuteuliwa.
Kamati hiyo ya Bunge pia ilipendekeza
kuwa waziri wa Nishati na Madini, waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, mwanasheria mkuu, katibu mkuu wa wizara ya
Nishati na Madini na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Tanesco
wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
Pia maazimio ya Kamati ya kudumu ya
bunge ilipendekeza kuwa, kwa miaka mingi mikataba mibovu ya kuzalisha
umeme kati ya Tanesco na makampuni binafsi imeisababishia Tanesco
hasara ya mabilioni ya fedha na kutishia uhai wake wa kifedha,
serikali iwasilishe mikataba husika bungeni au kwenye kamati zake kwa
lengo la kutekeleza vema wajibu wake wa kuimamia na kuishauri
serikali.
0 comments:
Post a Comment