WAY

Thursday, December 11, 2014

ZAIDI YA ASILIMIA 60 YA WATANZANIA WAMEJIANDIKISHA KUPIGGA KURA CHAGUZI SERIKALI ZA MITAA JUMAPILI TAR 14

Jumla ya watanzania milioni 11,491,661 sawa na asilimia 62 ya matarajio yaliyowekwa wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Aidha mkoa wa Dar -es-salaam umetajwa kufanya vibaya katika zoezi la uandikishaji huku mkoa wa Katavi ukiongoza kwa kufanya vizuri nchini.
                        Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Khalist Luanda

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma kuhusiana na kukamilika Kwa zoezi la uandikishwaji wa daftari la wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Khalist Luanda amesema katika zoezi hilo walitarajia kuandikisha wapiga kura wapatao milioni 18,587,742.


Amesema licha ya zoezi hilo kufanikiwa kwa zaidi ya nusu ya malengo ipo mikoa 2 na halmashauri mbili ambazo hazikufikia malengo na kuandikisha chini ya asilimia 50.

Ametaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam ambao uliandikisha asilimia 43 ya wapiga kura na mkoa wa Kilimanjaro ambao uliandikisha asilimia 50 ya wapiga kura.


Kwa upande wa halmashauri zilizofanya vibaya ni Kilindi iliyopo mkoani Tanga ambayo imeandikisha asilimia 21 na Halmashauri ya Wilaya ya Same iliyoandikisha asilimia 22.


Luanda ametaja mikoa miwili iliyofanya vizuri kuwa in Katavi ambao umevuka lengo Kwa kuandikisha asilimia 79 na ule wa Kagera ambao umevuka lengo Kwa kuandikisha asilimia 78 ya wapiga kura.


Ametaja halmashauri zilizofanya vizuri kuwa ni Mpanda ambayo imeandikisha asilimia 107 na kuvuka lengo pamoja na wilaya ya Babati ambao umeandikisha asilimia 101 ya wapiga kura na kuvuka lengo.


Akielezea utaratibu utakaotumika wa kupiga kura amesema ili kuthibitisha kuwa jina lililopo katika orodha ndilo la muhusika anayekuja kupiga kura watatumia vitambulisho aina nane ikiwemo cha kupigia kura, cha kazi, leseni na pasi ya kusafiria.


Ameviomba vyama vya siasa kutumia siku zilizobaki za kampeni kuhamasisha wanachama wao kujitokeza kupiga kura ili mafanikio yaliyopatikana katika zoezi la uandikishaji liende sambamba na upigaji kura na kusisitiza kuwa suala la ulinzi limeimarishwa.
MWISHO.
...................................
WATAKAOJARIBU KUVURUGA UCHAGUZI ARUSHA KUKIONA CHA MOTO.
Wananchi mkoani Arusha wameombwa kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwani serikali haitamvumilia mtu ama kikundi cha watu kitakachojaribu kuvuruga ama kutihishia amani wakati wa uchaguzi


                                 Mkuu wa mkoa wa Arusha Ndg, David Felix Ntibenda Kijiko
Tahadhari hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Arusha Bw. Felix Ntebenda Kijiko alipokuwa anazungumza na viongozi na watendaji wakati anapokelewa na kukabidhiwa ofisi na amewaomba wananchi wa Arusha kuacha kutumia nguvu na rasilimali zao kuvuruga amani badala yake washirikiane na serikali kukabiliana na mamtizo yaliyopo .


Amesema zipo taarifa za kuwepo kwa baadhi watu wanaojiandaa kuvuruga uchaguzi jambo alilodai kuwa halitapata nafasi na kusisitiza wananchi kujiepusha na mtu ama kikundi chochote cha watu kinajaribu kueneza ama kupanga njama hizo ..




Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Bw, Adostine Mapunda amesema kwa upande wa watumishi na watenaji wa halmashauri wamejipanga vizuri kuhakikihsa wanatoa ushirikiano wa kutosha kuwatumikia wananchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa zoezi la ujenzi wa maabara linakamilika.
MWISHO
..................................... 
UKAGUZI MABASI STAND MBEYA MADEREVA 3 WATIWA MBARONI KWA KUENDESHA WAKIWA WAMELEWA. 
Madereva watatu wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Mbeya na Dar es salaam wanashikiliwa na polisi Mkoani Mbeya, baada ya kukutwa wakijiandaa kusafirisha abiria wakiwa wamelewa,

               Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya,   Butusyo Mwambelo
Aidha mabasi mengine matatu pia yakitozwa faini na mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa majini na nchi kavu, sumatra kwa kosa la kutokuwa na madereva wawili pamoja na vibali vya kusafirisha abiria.


Jeshi la polisi kupitia kikosi cha usalama barabarani kwa kushirikiana na mamlaka ya usafiri wa nchi kavu na majini nchi sumatra jana alfajiri wamefanya ukaguzi wa kushtukiza katika kituo kikuu cha mabasi Jijini Mbeya na kuwabaini madereva hao watatu wakiwa wameshikilia usukani wa mabasi tayari kwa kusafirisha abiria huku wakiwa wamelewa chakari


Baada ya kuwatia mbaroni madereva hao, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mwambelo ametoa wito kwa wamiliki wa mabasi kutoajiri madereva walevi huku pia akiwaonya madereva kujiepusha na ulevi wakati wakiendesha magari.


Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafirishaji wa nchi kavu na majini Sumatra, Denis David amesema katika ukaguzi wake amebaini mabasi matatu yanayosafiri umbali mrefu yakiwa na dereva mmoja badala ya madereva wawili pamoja na basi moja ambalo halikuwa na leseni wala kibali cha kusafirisha abiria mkoani mbeya.
 MWISHO.
............................................. 
SERIKALI YAKUBALI YAISHE MGOGORO WA ARDHI MBALALI NA TANAPA.
Serikali imekubali kuachia maeneo ambayo yalipendekezwa yaingizwe kwenye hifadhi ya taifa ya Ruaha wilayani Mbarali ili kuondokana na mgogoro wa muda mrefu wa ardhi baina ya wakazi wanaozunguka hifadhi hiyo na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa TANAPA.
 
                            Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu ametoa tamko hilo wakati akizungumza na wandishi wa habari Mkoani Mbeya akisema kuwa maeneo ambayo yamekuwa na mgogoro kwa muda mrefu wilayani Mbarali baina ya wananchi na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa ni mali halali ya wananchi na sasa serikali imeamua kuachana nayo ili kumaliza migogoro hiyo.
 
Mbunge wa Mbarali, Modestus Dickson Kilufi amesema uamuzi huo wa Waziri Nyalandu umezingatia maslahi ya wananchi na kuwa sasa wananchi wataishi kwa amani wakishirikiana na Tanapa kuwalinda wanyama katika Hifadhi ya Ruaha.


Baadhi ya wananchi ambao wamehudhuria mkutano baina ya waziri na uongozi wa wilaya ya Mbarali wamesema wamefurahishwa na uamuzi huo wa serikali ambao utaleta mageuzi yasiyofutika kwenye maisha yao.

0 comments:

Post a Comment

.

.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...