SALAMU
ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA
DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,
TAREHE
31 DESEMBA, 2014
Utangulizi
Ndugu
zangu;
Watanzania
Wenzangu;
Kama
ilivyo ada imefikia siku ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha mwaka
mwingine. Leo tunauaga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2015.
Tunamshukuru Muumba wetu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na
kutuwezesha kuifikia siku ya leo. Kwa ndugu na jamaa zetu ambao
hawakujaliwa kuiona siku ya leo tuzidi kuwaombea mapumziko mema.
Nasi tumuombe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema atujaalie umri mrefu,
afya njema na mafanikio tele kwa kila tuliombalo katika mwaka 2015 na
miaka ijayo.
Ndugu
wananchi;
Hizi
ni salamu zangu za mwisho za mwaka mpya kutoa nikiwa Rais wa nchi
yetu. Mwakani salamu kama hizi zitatolewa na Rais wetu mpya. Mimi
wakati huo nitakuwa raia wa kawaida kijijini kwangu Msoga
nikifuatilia kwenye TV na radio hotuba ya Rais wa Awamu ya Tano ya
uongozi wa nchi yetu akitoa salamu zake za kwanza za mwaka mpya,
itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa kwangu.
Hali
ya Usalama
Ndugu
Wananchi;
Tunaumaliza
mwaka 2014 kwa salama na amani. Mipaka yetu iko salama na hakuna
tishio lolote la kiusalama kutoka ndani au nje ya nchi yetu. Uhusiano
wetu na nchi jirani na nyinginezo duniani ni mzuri. Hakuna nchi
iliyo adui au tunayoitilia shaka kuwa na njama za kuhatarisha usalama
wa Tanzania. Nawapongeza wanadiplomasia wetu pamoja na viongozi na
watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuifanya nchi
yetu kuwa salama.
Uhalifu
Unapungua
Ndugu
Wananchi;
Taarifa
za Polisi zinaonyesha kuwa, mwaka 2014 vitendo vya uhalifu vimepungua
ikilinganishwa na mwaka 2013. Mwaka huu, matukio ya uhalifu
yaliyoripotiwa
Polisi
yalikuwa 64,088
ikilinganishwa na matukio 66,906
katika
mwaka 2013. Haya ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la
Polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja na raia
wema. Naomba ushirikiano huu uendelee mwaka ujao na miaka ijayo ili
tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi.
Ajali
za Barabarani
Ndugu
Wananchi;
Nimefarijika
kusikia pia kuwa matukio ya ajali za barabarani nchini nayo
yanaendelea kupungua. Mwaka huu kumetokea ajali 14,048
zilizosababisha vifo vya watu 3,534
na wengine 16,166
kujeruhiwa. Mwaka 2013 kulitokea ajali 22,383
zilizosababisha vifo 3,746
na majeruhi 19,433.
Hivyo mwaka huu kulikuwa na ajali 8,335,
vifo
212 na
majeruhi
3,267
pungufu kuliko mwaka jana. Huu ni mwelekeo mzuri na wa kutia moyo
ingawa bado ni nyingi mno. Naomba yale tuliyoyafanya yaliyotuwezesha
kupata unafuu huu mwaka huu yaendelezwe maradufu mwaka 2015 na miaka
ijayo.
Ugaidi
Ndugu
Wananchi;
Mwaka
huu tumefanikiwa kutambua mtandao wa viongozi na washirika wao
wanaotuhumiwa kupanga na kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia
mabomu na kumwagia watu tindikali Tanzania Bara na Zanzibar. Watu
112
wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wametiwa nguvuni.
Tayari watuhumiwa 87
kati yao wameshafikishwa mahakamani na waliosalia watafikishwa wakati
wo wote. Uchunguzi unaendelea ili kuwatambua wahusika wengine ambao
hawajakamatwa.
Ndugu
wananchi;
Kwa
niaba ya Watanzania wenzangu wote, natoa pongezi nyingi kwa vyombo
vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyofanya ya kutambua
mtandao wa ugaidi nchini na kuchukua hatua thabiti za kuudhibiti.
Hali kadhalika nawashukuru raia wema waliotoa taarifa zilizowezesha
haya kufanyika. Hatupaswi kubweteka wala kudhani kuwa mambo
yamekwisha. Lazima tuendelee kuchukua tahadhari muda wote kwani
hatujui adui anapanga kufanya hujuma gani, lini na wapi.
Dawa
za Kulevya
Ndugu
Wananchi;
Tumeendelea
kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya biashara na
matumizi ya dawa za kulevya nchini. Mwaka huu watuhumiwa 935
wakiwemo
vigogo wa biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya kesi 19
zimefunguliwa Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo
400
za heroine, kilo 45
za cocaine na kilo
81,318
za bangi zimekamatwa. Narudia kutoa pongezi nyingi kwa Kikosi Kazi
Maalum cha Kukabiliana na dawa za kulevya nchini kwa mafanikio
yanayoendelea kupatikana. Matunda ya kazi yao tunayaona. Naomba
juhudi ziongezwe maradufu mwaka ujao na miaka ijayo. Serikali
itaendelea kuwaunga mkono.
Ndugu
wananchi;
Kama
nilivyoahidi mwaka jana, Muswada wa Sheria ya Kuthibiti na Kupambana
na Dawa za Kulevya umeshasomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa
Novemba, 2014 wa Bunge letu tukufu. Pamoja na kupendekeza kuongeza
adhabu kwa makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, Muswada huo pia
unapendekeza kuanzisha chombo kipya chenye nguvu cha kuzuia na
kupambana na dawa za kulevya. Muswada huu ukipitishwa na kuwa Sheria
tutakuwa tumeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya biashara na matumizi
ya dawa za kulevya nchini.
Ujangili
wa Wanyamapori
Ndugu
Wananchi;
Katika
mwaka tunaomaliza leo mapambano dhidi ya
ujangili
na biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori
yameimarishwa. Kwa ujumla kasi ya ujangili imeendelea kupungua.
Katika mwaka 2014 ndovu 114
waliuawa ikilinganishwa na ndovu 219
waliouawa mwaka 2013 au ndovu 473
mwaka 2012. Aidha, majangili 1,354
wamekamatwa na pembe za ndovu 542
na silaha mbalimbali 184
nazo zilikamatwa. Naamini uamuzi wa kuifanya Idara ya Wanyamapori
katika Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Wakala yaani Tanzania
Wildlife Agency
(TAWA) kutaongeza nguvu ya kuhifadhi wanyama pori na mapambano dhidi
ya ujangili.
Natoa
pongezi nyingi kwa askari wa wanyamapori, Jeshi la Polisi na vyombo
vingine vya Serikali na raia wema kwa kazi nzuri wanayoendelea
kufanya na mafanikio yanayoendelea kupatikana. Juhudi za kupambana
na ujangili na biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori
zitaendelezwa kwa nguvu zaidi mwaka ujao 2015 na miaka inayofuatia.
Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati marafiki zetu wa
maendeleo wanaotuunga mkono kwa hali na mali katika mapambano haya.
Naomba waendelee kutusaidia.
Hali
ya Uchumi Jumla
Ndugu
wananchi;
Mwaka
2014 ulikuwa mzuri kwa uchumi wa taifa. Uzalishaji katika sekta
nyingi ulikuwa ni mzuri. Ndiyo maana tunategemea kuwa tutafikia au
hata kuvuka lengo tulilojiwekea la pato la taifa kukua kwa asilimia
7.4
mwaka huu. Mwaka 2013 pato la taifa lilikua kwa asilimia
7.3.
Mfumuko wa bei uliendelea kushuka na kufikia asilimia
5.8 Novemba,
2014 ukilinganisha na Januari 2014 ulipokuwa asilimia
6.0.
Hali nzuri ya upatikanaji wa chakula nchini imesaidia sana kufanya
mfumuko wa bei kuendelea kushuka. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko wa
bei utaendelea kushuka na kufikia asilimia
5 ifikapo
Juni, 2015.
Mauzo
Nje
Ndugu
Wananchi;
Mauzo
nje yameendelea kuongezeka. Katika kipindi kilichoishia Oktoba 31,
2014, Tanzania iliuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za
Marekani milioni
8,503.9
ukilinganisha
na mauzo ya dola milioni
8,332.5
katika
kipindi kama hicho mwaka
2013. Mapato yetu yangekuwa makubwa zaidi kama bei za kahawa, chai,
korosho na pamba zisingeanguka au bei ya dhahabu nayo isingepada.
Akiba
ya Fedha za Kigeni
Ndugu
Wananchi;
Akiba
yetu ya fedha za kigeni ilikuwa Dola za Marekani milioni
4,251.8 kwa
kipindi kilichoishia
Novemba 30, 2014. Kiasi hicho kinatuwezesha kuagiza bidhaa toka nje
kwa miezi 4.1.
Hii ni chini ya lengo letu la kuwa na akiba ya fedha za kigeni ya
kuagiza bidhaa kwa miezi minne
na nusu.
Hata
hivyo,
sina
wasiwasi kabisa kwamba tofauti hii ndogo tutaweza kuiziba mwaka 2015.
Mapato
ya Serikali
Ndugu
Wananchi;
Makusanyo
ya mapato ya Serikali kwa mwezi, kati ya Julai hadi Novemba, 2014
yaliongezeka kutoka shilingi bilioni
3,555.5
kipindi kama hicho mwaka 2013 hadi shilingi bilioni
3,924.1
mwaka huu. Hata hivyo, makusanyo hayo yalikuwa asilimia
90
ya lengo tulilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni
4,459.7.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato, zipo sababu mbalimbali
zilizosababisha lengo lisifikiwe katika nusu ya kwanza ya mwaka wa
fedha wa 2014/2015. Hatua zipasazo zinaendelea kuchukuliwa
kurekebisha mambo hayo ili katika nusu ya pili ya mwaka huu wa fedha
makusanyo yafikie lengo na ikiwezekana yazidi ili kufidia pengo la
nusu ya kwanza.
Takwimu
Mpya za Pato la Taifa
Ndugu
wananchi,
Ni
utaratibu wa kawaida wa nchi zote duniani kuwa na mwaka unaotumika
kuwa kizio (base year) cha kukokotoa takwimu za Pato la Taifa. Ni
utaratibu wa kawaida pia kwa kila baada ya muda fulani mwaka wa kizio
hubadilishwa. Lengo ni kuboresha takwimu husika. Katika marekebisho
hayo pia huingizwa thamani ya bidhaa na huduma mpya katika pato la
taifa na kuziondoa zilizotoweka ili kutoa picha halisi ya ukuaji wa
shughuli za kiuchumi.
Katika
miaka ya hivi karibuni nchi za Ghana (mwaka 2010), Nigeria (mwaka
2013) na Kenya (mwaka 2014) wamefanya marekebisho ya takwimu zao za
pato la taifa. Na sisi Tanzania tumefanya hivyo mwaka huu (2014).
Hii ni mara ya tano kwa nchi yetu kurekebisha takwimu za pato la
taifa. Mara nne zilizopita ilikuwa mwaka 1966, 1976, 1992 na 2001.
Ndugu
wananchi;
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imekamilisha marekebisho ya takwimu za pato la
taifa na kukokotoa takwimu mpya kwa kutumia mwaka 2007 kama mwaka wa
kizio. Kutokana na marekebisho yaliyofanyika, pato la taifa kwa
mwaka 2013 ni shilingi
trilioni
70
kwa
kutumia bei za mwaka 2007. Ukitumia bei za mwaka 2001, pato la taifa
kwa mwaka 2013 ni shilingi
trilioni 53.17.
Kuongezeka kwa pato la taifa kumeongeza pia pato la wastani la kila
Mtanzania kutoka shilingi
1,186,200
(sawa na US$
742)
kwa bei za mwaka 2001 hadi shilingi
1,560,050
(sawa na US$
977)
kwa bei za mwaka 2007.
Kilimo
na Chakula
Ndugu
Wananchi;
Mwaka
2014 ulikuwa mzuri sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini.
Uzalishaji ulikuwa tani milioni
16.02
ukilinganisha na uzalishaji wa tani milioni
14.38
mwaka wa jana 2013.
Hili
ni ongezeko la tani milioni
1.64.
Kwa mujibu wa mahitaji yetu ya chakula nchini kuna ziada ya tani
milioni 3.25. Katika
ziada hiyo, mahindi yanachangia tani
milioni 1.55,
mchele
tani 794,000
na kiasi kinachobakia kinachangiwa na mazao mengine ya chakula.
Ndugu
wananchi;
Kuna
jambo moja muhimu kuhusu ununuzi wa nafaka ambalo ningependa
kulifafanua. Naomba ieleweke kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) sio mnunuzi wa mahindi yote, mpunga wote na mtama
wote unaozalishwa na wakulima nchini. Wakala hununua sehemu ndogo
tu ya nafaka ya ziada iliyozalishwa na hununua kwa ajili ya kuweka
akiba ya taifa ya chakula cha kutumika wakati wa dharura ya watu
kupata tatizo la njaa. Aidha, Wakala hununua kiasi kinacholingana na
uwezo wa maghala yake kuhifadhi. Kwa sasa uwezo wa maghala yetu ni
kuhifadhi tani
246,000 ingawaje
tunaendelea kujenga maghala mengine mpaka tufikie uwezo wa kuhifadhi
tani
400,000 ifikapo
2015.
Hivyo
basi kwa Wakala kununua
tani 292,415.41 mwaka
huu ina
maana kwamba kiasi cha karibu tani
50,000
zinahifadhiwa nje ya maghala kwa kutumia maturubai. Huu siyo
utaratibu mzuri na haifai kuendelea nao kwani kuna hatari ya nafaka
hiyo kuharibika na kuzua mgogoro mkubwa siku moja.
Ndugu
wananchi;
Baada
ya NFRA kununua tani
292,415.41
kuna takribani tani
milioni
2.96
za nafaka ya ziada ambayo iliyobaki mikononi mwa wakulima. Mategemeo
yetu ni kuwa wafanyabiashara wetu watanunua nafaka hiyo kwa ajili ya
kuuza mijini na kwingineko inakohitajika. Bahati mbaya mwaka huu
kama ilivyokuwa mwaka wa jana, wafanyabiashara wetu hawakuweza
kununua nafaka yote ya ziada ambayo Serikali haikuweza kununua
kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Hali hii imezua tatizo
ambalo Serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara nchini hatuna
budi kulitafutia majawabu. Tunalazimika kutafuta masoko mengine
ndani na hata nje ya nchi ya kuuza mahindi, mpunga na mtama wa ziada.
Nimeagiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda
na Biashara kukaa chini na kushirikiana na wafanyabiashara
kulitafutia ufumbuzi suala hili lenye maslahi makubwa kwa wakulima na
nchi yetu kwa jumla.
Ndugu
Wananchi;
Katika
mazingira haya, ninapopata taarifa ya kuwepo watu wanaotaka kuuza
mahindi nje ya nchi lakini wanawekewa vikwazo na maafisa wa Serikali
inanishangaza na kunisikitisha. Nawataka wale wote wanaofanya hivyo
waache mara moja na badala yake wawasaidie wafanyabiashara hao
kufanikisha azma yao. Hali kadhalika, tuwashawishi watu wengine nao
wajitokeze kufanya biashara hiyo. Jambo muhimu ninalopenda
kulisisitiza ni kwamba pawepo na utaratibu mzuri ili biashara hiyo
ifanywe kwa kutumia njia halali na zilizo wazi. Kutumia njia za
panya hakukubaliki na wala hakuna sababu ya kufanya hivyo.
Miradi
ya Kimkakati
Ndugu
wananchi;
Katika
mwaka 2014 utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa mujibu wa
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) umeendelea
vizuri. Tunayo matumaini makubwa kwamba katika mwaka 2015 miradi
mingi itakamilika.
Tuanze
na Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo hadi
Dar es Salaam. Mradi huu unategemewa kukamilika Januari, 2015.
Utakapokamilika utatuwezesha kutimiza lengo letu la kuzalisha MW
2,780 za
umeme
ifikapo 2016. Mipango ya kupata ardhi ya ujenzi wa mitambo ya
kuchakata gesi asili kuwa ya kumiminika (LNG) ili iweze kusafirishwa
kwenda kwenye masoko, inakwenda vizuri.
Ndugu
Wananchi;
Utekelezaji
wa mradi mkubwa wa kimkakati wa kusambaza umeme vijijini umeendelea
vizuri na tumepata mafanikio makubwa yasiyokuwa na mfano wake katika
historia ya nchi yetu. Hadi kufikia Novemba, 2014, jumla ya vijiji
3,836
vimepatiwa umeme na vingine 1,500
vinategemewa kupatiwa umeme ifikapo Juni, 2015. Hivyo basi, vijiji
5,336
kati ya vijiji 12,423
vya Tanzania Bara vitakuwa vimepatiwa umeme. Hii ni sawa na asilimia
43
ya vijiji vyote nchini vitavyokuwa vimepata umeme. Hivi sasa
wananchi milioni
17.3 nchi
nzima sawa asilimia
36
wamefikiwa na huduma ya umeme ikilinganishwa na watu milioni
8.1
sawa na asilimia
18.4
waliokuwa wamefikiwa na huduma hiyo mwaka 2012. Mwaka 2015
tunatarajia watu milioni
18.2
sawa na asilimia
38
watafikiwa na umeme. Kwa upande wa vijijini mwaka 2012 watu milioni
2.3 sawa
na asilimia
7
walikuwa na umeme. Ifikapo Juni 2015, idadi hiyo itaongezeka na kuwa
milioni
7.4
sawa na asilimia
21.
Haya ni mafanikio makubwa kwa wananchi wengi vijijini na mijini
kupata umeme katika kipindi kifupi kiasi hiki. Ni mageuzi ya aina
yake yatokayotoa mchango muhimu katika kuinua hali za maisha ya
Watanzania.
Ndugu
Wananchi;
Tunaanza
kuiona nuru ya matumaini kwamba siku si nyingi kutoka sasa, makaa ya
mawe ya Mchuchuma na madini ya chuma ya Liganga yataweza kutumika kwa
maendeleo ya nchi yetu na watu wa Ludewa. Maandalizi yote muhimu
yamekamilika kwa ajili ya Januari, 2015 kuanza ujenzi wa mgodi wa
makaa ya mawe kule Mchuchuma, mtambo wa kufua umeme, ujenzi wa mgodi
wa chuma kisichoyeyushwa pale Liganga na ujenzi wa kiwanda cha
kuyeyusha chuma.
Natoa
pongezi maalum kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na wabia
wenzao, Kampuni ya Sichuan Hongda ya China kwa hatua iliyofikiwa.
Inakadiriwa kuwa miradi hii ikikamilika itatoa ajira 33,000
za
moja kwa moja na zisizokuwa za moja kwa moja.
Ndugu
Wananchi;
Mradi
mwingine mkubwa wa kimkakati ni ule wa kujenga Eneo Maalumu la
Kiuchumi (Special Economic Zone) la Mbegani, Bagamoyo. Kwa mujibu wa
mpango kazi wa wabia wa mradi huo yaani Mamlaka ya Kuendeleza Maeneo
huru ya Uwekezaji (EPZA), Kampuni
ya China
Merchants Holdings International na
Mfuko wa Uhifadhi wa Akiba ya Mali za Serikali ya Oman (Oman State
General Reserve Fund), ujenzi wa bandari na miundombinu mingine
itakayowezesha viwanda kujengwa imepangwa kuanza Julai 2015.
Miundombinu
ya Usafiri na Uchukuzi
Ndugu
Wananchi;
Katika
mwaka huu wa 2014 kazi ya kujenga barabara za lami na kuimarisha
barabara za udongo ili ziweze kupitika wakati wote ziliendelea kote
nchini. Huu nao ni mradi mkubwa wa kimkakati. Barabara za lami 19
zenye urefu wa kilometa
1,459
zimekamilika kujengwa mwaka huu katika Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Rukwa,
Kagera, Dar es Salaam, Dodoma, Tanga, Morogoro, Arusha, Tabora na
Shinyanga. Ujenzi unaendelea kwa barabara nyingine 24
katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Rukwa, Simiyu,
Katavi, Tabora, Mwanza, Dar es Salaam, Kagera na Pwani ambazo wakati
wo wote mwaka 2015 zitakamilika. Maandalizi ya kuanza ujenzi wa
barabara nyingine nane
yanaendelea vizuri sehemu mbalimbali nchini.
Kwa
kutumia fedha za Mfuko wa Barabara, tumeendelea kufanya kazi ya
ujenzi na ukarabati wa barabara za udongo kote nchini. Mwaka huu
Mfuko huo umetengewa shilingi
bilioni 751.7
ukilinganisha na shilingi
bilioni 504.4
mwaka jana. Aidha, mwaka huu tumeweka jiwe la msingi la ujenzi wa
Daraja la Mto Kilombero. Matumini yetu ni kuwa ujenzi wa daraja hilo
na Daraja la Kigamboni utakamilika mwaka 2015. Ujenzi wa Daraja la
Malagarasi ulishakamilika mwaka jana, kinachosubiriwa ni sherehe ya
uzinduzi.
Kwa
upande wa jiji la Dar es Salaam, tunategemea kukamilisha ujenzi wa
Awamu ya Kwanza ya barabara za mabasi yaendayo kasi. Ni matarajio
yetu pia kwamba mabasi yataanza kusafirisha abiria katika kipindi cha
nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Halikadhalika, tunategemea katika
mwaka 2015 ujenzi utaanza wa barabara zinazozunguka jiji la Dar es
Salaam (ring roads), barabara ya Mwenge - Morocco na ile ipitayo juu
ya nyingine (flyovers) eneo la TAZARA. Vile vile, daraja jipya la
Salenda litaanza kujengwa. Aidha, kivuko cha abiria 300
cha MV Dar es Salaam kitaanza kusafirisha abiria kati ya Dar es
Salaam Kaskazini na Ferry mapema mwakani. Hatua zote hizi zinalenga
kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Usafiri
wa Anga na Reli
Ndugu
wananchi;
Jitihada
za kuboresha huduma ya usafiri katika Reli ya Kati zimeendelea kwa
mafanikio. Mwaka huu vichwa vinane
vya treni vimekarabatiwa, mabehewa mapya 22
ya abiria na mabehewa 274
ya mzigo yamenunuliwa. Mabehewa hayo yameanza kuwasili nchini kati ya
Novemba na Desemba mwaka huu. Kati ya Januari na Mei, 2015
tunatarajia kupokea vichwa vipya vya treni 13.
Uboreshaji huu wa huduma za treni unakwenda sambamba na ukarabati wa
reli yenyewe, ujenzi wa madaraja na kuimarisha maeneo yaliyo korofi
katika reli hiyo.
Kuhusu
ujenzi wa reli iliyo pana zaidi (standard guage), yenye uwezo wa
kubeba mabehewa mengi na kuwezesha treni kwenda kwa mwendo wa kasi
zaidi, juhudi za kutafuta fedha za ujenzi au wabia wa kushirikiana
nasi kujenga zinaendelea. Wakati huo huo, tunaendelea na juhudi za
kutafuta ufumbuzi kwa matatizo ya reli ya TAZARA ili mambo yaende
vizuri. Tutashirikiana kwa karibu na wabia wenzetu wa Zambia. Bahati
nzuri Serikali ya China iko tayari kuunga mkono juhudi zetu za
kufufua reli ya TAZARA.
Usafiri
wa Anga
Ndugu
Wananchi;
Sekta
ya usafiri wa anga imeendelea kukua katika mwaka 2014. Idadi ya
abiria wanaowasili na kutoka katika viwanja vyetu vya ndege nchini
imeongezeka kutoka abiria milioni
2.5
mwaka 2013 hadi abiria milioni
3.5
kufikia
Septemba, 2014. Safari za ndege kati ya Tanzania na nchi za nje
zimeongezeka kutoka 274
Januari, 2013 hadi 295
kufikia Septemba, 2014. Hili ni ongezeko la asilimia
8.
Safari za ndege ndani ya nchi nazo zimeongezeka kutoka safari 230,458
mwaka 2013 hadi safari 241,922
mwaka 2014. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia
39.
Maongezeko haya ni kielelezo na ushahidi kuwa shughuli za utalii na
biashara nchini zimeendelea kukua.
Ndugu
Wananchi;
Ujenzi
wa Jengo la 3
(Terminal
3)
la
Abiria
katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere unaendelea vizuri.
Jengo hilo litakapokamilika mwakani, litakuwa na uwezo wa kuhudumia
wastani wa abiria milioni
8
kwa mwaka. Aidha, ukarabati wa Jengo la 2
(Terminal 2)
utafanyika ili liweze kutoa huduma iliyo bora zaidi. Sambamba na
ujenzi huo, Wakala wa Viwanja vya Ndege wameendelea kukarabati na
kuboresha viwanja vya ndege vya KIA,
Mwanza, Songwe, Bukoba, Tabora
na Kigoma.
Tunatarajia ukarabati wa viwanja vya ndege vya Shinyanga
na
Sumbawanga
kuanza
mapema
mwaka 2015.
Elimu
Ndugu
wananchi;
Tumeendelea
kupiga hatua za kuridhisha katika kuboresha elimu nchini.
Tumefanikiwa kupunguza tatizo la upungufu wa maabara, vitabu na
walimu wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tumeajiri walimu
36,339
kati ya 81,562
wanaohitajika. Tumebakiwa na upungufu wa walimu
45,223 yaani
26,946
wa
shule za msingi na
18,277
wa
shule za
sekondari
hususan wa masomo ya sayansi.
Hivi sasa hatuna tatizo la walimu wa masomo ya sanaa katika shule za
sekondari.
Mwaka
huu tumeanza
mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya Diploma ya Ualimu kwa masomo ya
sayansi na hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo jumla ya
wanafunzi 5,602
wa masomo hayo wamedahiliwa.
Mpango huu utatuwezesha kupunguza pengo kubwa tulilonalo la walimu wa
sayansi katika muda mfupi zaidi.
Ujenzi
wa Maabara
Ndugu
wananchi;
Ujenzi
wa maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za sekondari
za Kata 3,463
umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shule inatakiwa zijengwe
maabara 10,389
ilipofika Novemba, 2014. Taarifa kutoka TAMISEMI zinaonyesha kuwa
hadi kufikia Desemba 29, 2014, maabara 4,207
sawa na asilimia
40.5
zilikuwa zimekamilika, maabara 5,688
sawa na asilimia
54.8
zilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji, na maabara 494
sawa na asilimia
4.
zilikuwa katika hatua za awali za ujenzi.
Ndugu
Wananchi;
Natoa
pongezi nyingi kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti na
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji nchini pamoja
na wananchi, kwa jitihada kubwa iliyofanyika. Kwa kutambua jitihada
hizo, nimeongeza miezi
sita
zaidi kwa wale ambao hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo wafanye
hivyo. Sikusudii kuongeza tena muda baada ya hapo. Naomba watumie
kipindi hicho kitumike kutafuta vifaa vya maabara. Serikali itasaidia
upatikanaji wa watunza maabara (laboratory
technicians)
ambao tumeanza programu kubwa ya mafunzo yao na mahitaji mengine ya
maabara.
Ununuzi
wa Vitabu
Ndugu
Wananchi;
Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya
kufundishia katika shule za msingi na sekondari. Tumekuwa tunanunua
vitabu kwa kutumia Bajeti ya Serikali na misaada kutoka kwa marafiki
zetu wa maendeleo. Kwa mfano, Serikali ya Marekani imetupatia vitabu
milioni
2.5
vya masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari. Ongezeko
hili la vitabu linashusha uwiano uliopo sasa wa kitabu
kimoja
kwa wanafunzi
wanne
na kufikia kitabu
kimoja
kwa wanafunzi
wawili.
Lengo letu ni kila mtoto kuwa na kitabu chake kwa kila somo ifikapo
mwaka 2016.
Sera
Mpya ya Elimu na Mafunzo
Ndugu
wananchi;
Mafanikio
mengine tuliyopata mwaka huu ni kukamilika kwa Sera ya Elimu na
Mafunzo ya mwaka 2014. Hii ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya
elimu nchini hakuna badala yake. Sera
mpya inalenga kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na
taratibu zitakazowezesha Watanzania
wengi zaidi kupata fursa za elimu iliyo bora na inayolinga na wakati
tulionao. Jambo jipya sana na la kihistoria katika Sera mpya ya
Elimu ni dhamira ya Serikali ya kuondoa ada katika elimu ya sekondari
kuanzia mwaka 2016. Mpaka sasa hatuna ada kwenye shule za msingi,
sasa wakati umefika kufanya hivyo pia kwa elimu ya sekondari. Kwa
mujibu wa maelezo hayo ya Sera, nimekwishatoa maagizo kwa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango kuanza kutafakari namna
jambo hilo litakavyotekelezwa.
Afya
Ndugu
Wananchi;
Katika
mwaka 2014 jitihada za kuboresha huduma ya afya kwa Watanzania
ziliendelea. Tulipambana kwa mafanikio na mlipuko wa homa ya dengue
iliyowapata watu 1,039
na kusababisha vifo vya watu 3
kati
yao. Kwa upande wa maradhi ya ebola tumejiandaa vya kutosha kutambua
watu wenye maradhi hayo wanapoingia nchini kupitia viwanja vya ndege
vya kimataifa na vituo vyote vya mpakani. Aidha, tumejipanga vyema
kuwahudumia wagonjwa wa maradhi hayo iwapo watatokea.
Mwaka
huu pia, Madaktari wetu watano
wamekwenda Liberia kusaidiana na ndugu zetu wa huko katika
kukabiliana na ugonjwa wa ebola. Madaktari wetu hao wako salama na
wanaendelea vizuri kutoa huduma. Madaktari hao watakaporejea nchini
watakuwa hazina kubwa ya taifa katika kupanga mipango ya kukabiliana
na ugonjwa huu hatari. Hali kadhalika, watakuwa viongozi wa wengine
katika kutibu wagonjwa wa maradhi ya ebola iwapo watatokea nchini.
Ndugu
Wananchi;
Katika
kipindi cha Januari hadi Desemba, 2014, tumeweza kuajiri watumishi wa
sekta ya afya 8,345
ambao kati yao kuna madaktari 244,
madaktari bingwa 75,
wauguzi 2,555
na wataalamu wa kada nyingine za afya 5,471.
Mwaka huu pia tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka
wanafunzi 7,956
katika mwaka 2012/2013 hadi wanafunzi 9,730.
Kwa
ongezeko hilo, sasa tumefikia asilimia
97
ya lengo letu la kudahili wanafunzi 10,000
ifikapo mwaka 2017.
Jitihada zetu za
kuongeza fursa za mafunzo kwa Madaktari, Wauguzi na wataalamu wengine
wa afya zina muelekeo mzuri. Ujenzi wa hospitali ya kufundishia pale
Mloganzila unaendelea vizuri na hospitali ya kufundishia ya Chuo
Kikuu cha Dodoma umekamilika. Ni matarajio yangu kuwa wakati wo wote
mwakani ujenzi wa kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Muhimbili pale
Mloganzila utaanza. Ujenzi huo ukikamilika Chuo kikuu cha Muhimbili
kitaweza kudahili wanafunzi
12,000 kutoka
wanafunzi
2,500
wa sasa jambo ambalo litafanya upungufu wa Madaktari, Wauguzi na
Wataalamu wa Afya kupata jawabu la uhakika. Tumeendelea kufanya mambo
mengine ikiwemo ujenzi wa jengo la tiba za ubongo na mishipa ambalo
limekamilika pale Muhimbili, sasa tunahangaikia kupata vifaa.
Maji
Ndugu
Wananchi;
Katika
mwaka huu wa 2014 tumeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya
kuwapatia wananchi maji safi na salama mijini na vijijini. Kwa ajili
hiyo miradi 498
ya maji vijijini imekamilika na miradi 740
ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Miradi mingine 378
ipo katika maandalizi ya ujenzi kuanza. Ni matarajio yetu kwamba
katika mwaka ujao wa 2015, miradi mingine 731
itatekelezwa na vituo 25,790
vya kuchota maji vitajengwa. Miradi hii ikikamilika tutaweza
kuwafikia asilimia
71 ya
wananchi wanaopata maji safi na salama vijijini kutoka asilimia
58
ya sasa. Kwa ajili hiyo, tutakuwa tumevuka lengo tulilojiwekea la
kuwapatia watu maji asilimia
65
ya Watanzania waishio vijijini ifikapo 2015. Ombi langu kwa ndugu
zetu wa Hazina waiangalie sekta hii ya maji kwa ukaribu zaidi na
wawapatie fedha kwa wakati.
Ndugu
Wananchi;
Utekelezaji
wa mradi wa kuipatia maji miji ya Mwanga
– Same – Mkomazi pamoja
na miji na vijiji vyote vya njiani, utaanza Februari, 2015. Fedha
zimekwishapatikana na Mkandarasi wa Awamu ya Kwanza ameshapatikana.
Makandarasi wa Awamu ya Pili na Tatu watapatikana muda si mrefu
kutoka sasa. Hii pia itahusu kupata Mkandarasi wa mradi wa maji wa
mji wa Orkesment.
Ndugu
Wananchi;
Mwaka
huu miradi ya kuipatia maji miji kadhaa nchini ilikamilika na tatizo
la upungufu wa maji litakuwa limepatiwa ufumbuzi. Ipo miji kadhaa
ambayo miradi imefikia hatua ya juu na kwamba wakati wowote mwakani
itakamilika. Jiji la Dar es Salaam lipo katika kundi hili. Kazi ya
upanuzi wa miradi ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kwa msaada wa
Serikali ya Marekani na mkopo kutoka Serikali ya India imefikia hatua
nzuri. Inatarajiwa kukamilika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2015.
Mwaka ujao pia visima virefu vya Kimbiji na Kipera vitachimbwa na
Bwawa la Kidunda litaanza kujengwa.
Serikali
ya India pia imekubali kutupatia mkopo wa Dola
za Marekani milioni 268.2
kwa ajili ya kugharamia mradi wa kuipatia maji miji ya Tabora, Nzega
na Igunga kutoka Ziwa Victoria. Uwezekano wa kujumuisha miji ya
Sikonge na Urambo katika mradi huo utaangaliwa.
Bunge
na Mahakama
Ndugu
Wananchi;
Katika
mwaka 2014, mihimili ya Bunge na Mahakama iliendelea kutekeleza vyema
majukumu yao. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeweza
kuendesha shughuli zake kama ilivyopangwa pamoja na kulazimika
kugawana Ukumbi ule wa Bunge na Bunge Maalum la Katiba. Bunge
limefanya mikutano mitatu,
Miswada 17
ya Sheria ilisomwa kwa mara ya kwanza, Sheria tano
na maazimio saba
yalipitishwa. Maswali ya msingi 569
na ya nyongeza 1,541yaliulizwa
na kujibiwa. Aidha,
sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow nalo lilijadiliwa na kutolewa
maazimio.
Tumeshaanza kuchukua hatua kuhusu maazimio hayo na bado tunaendelea.
Napenda
kuitumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Wabunge wetu kwa
kutekeleza vizuri wajibu wao wa Kutunga Sheria na kusimamia Serikali.
Nawasihi waendelee na msimamo huo mwema na chanya kwa maslahi ya
nchi yetu na watu wake.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
upande wa Mahakama napenda kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa
ya kupunguza mrundikano wa mashauri katika Mahakama za ngazi zote.
Wahenga wamesema “mcheza
kwao hutunzwa”.
Hatuna budi kutoa pongezi maalum kwa Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed
Chande Othman kwa uongozi wake mahiri. Chini ya uongozi wake Majaji
wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi na
Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wamejiwekea malengo ya kusikiliza na
kutoa hukumu kwa mashauri yasiyopungua 200
kwa
mwaka kila mmoja wao.
Habari
njema na ya kuleta faraja ni kwamba utekelezaji unaendelea vizuri.
Mashauri 870
yalisikilizwa
na kuamuliwa kwenye Mahakama ya Rufani, mashauri 11,334
kwenye Mahakama Kuu, mashauri 8,715
kwenye Mahakama ya Mahakimu Wakazi na Mashauri 25,683
katika Mahakama za Wilaya. Aidha, mkakati wa kupeleka timu ya
Majaji wa Mahakama Kuu kwa wakati mmoja kwenye maeneo yenye mashauri
mengi kama ilivyofanyika Kigoma, Shinyanga na Tabora umesaidia sana
kupunguza mrundikano wa mashauri ya siku nyingi. Haijawahi kutokea
mashauri mengi kiasi hicho kusikilizwa na kumalizwa katika historia
ya Mahakama nchini.
Ndugu
Wananchi;
Mkakati
huu mpya umeleta matumaini mapya kwamba tatizo la kuchelewesha kwa
mashauri ambalo lilidhaniwa kuwa ni tatizo sugu sasa limeanza
kupatiwa ufumbuzi. Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote natoa
shukrani na pongezi nyingi kwa Jaji Mkuu, Majaji wa Rufani, Jaji
Kiongozi, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu wa ngazi zote kwa kazi
nzuri waifanyayo.
Hali
kadhalika, nampongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama na watendaji wote wa
Mahakama kwa kazi nzuri waifanyayo ya kuwawezesha Majaji na Mahakimu
kutimiza ipasavyo majukumu yao. Hakika utendaji Mahakamani
umebadilika na kuwa bora zaidi. Mimi naahidi kuendelea kusaidia
Mahakama kwa kuwahimiza ndugu zetu wa Hazina kutoa kwa wakati pesa
zilizotengwa katika bajeti.
Mapambano
Dhidi ya Rushwa
Ndugu
Wananchi;
Mapambano
dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka yameendelea bila ya
ajizi. Katika mwaka huu wa 2014 TAKUKURU wamepokea taarifa 237
na
wamekamilisha uchunguzi wa mashauri 545.
Watuhumiwa waliofikishwa Mahakamani ni 428.
Mashauri yaliyomalizika ni 205,
kati ya hayo 125
watuhumiwa waliachiliwa na 80
walipatikana na hatia na kuhukumiwa. Mwaka huu wa 2014 mali na fedha
taslimu zenye thamani ya shilingi
bilioni 38.96
zimeokolewa. Katika kuimarisha Taasisi hiyo kiutendaji, maafisa
wapya 394
wameajiriwa.
Sherehe
za Miaka 50 ya Muungano
Ndugu
Wananchi;
Mwaka
huu wa 2014 tuliadhimisha miaka 50 ya Muungano wa nchi zetu mbili
yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kwa
heshima inayostahili. Maadhimisho yalifikia kilele tarehe 26 Aprili,
2014 na zilifanyika sherehe nchini kote na sherehe hizo zilifana
sana. Ni ukweli usiopingika kuwa kwa Muungano wetu kuweza kudumu kwa
nusu karne ukiwa bado imara na unazidi kustawi ni mafanikio makubwa.
Matumaini kwa siku za usoni ni mazuri. Naamini Muungano wetu
utaimarika zaidi iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa kwani yale
mambo yenye kuleta matatizo hivi sasa yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.
Miaka
50 ya JWTZ
Ndugu
Wananchi;
Wakati
nchi inasherehekea miaka 50 ya Muungano, baadhi ya vyombo na taasisi
muhimu kitaifa zilifanya hivyo hivyo. Miongoni mwa walioadhimisha
nusu karne ya kuundwa kwake ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania kama mjuavyo JWTZ ilizaliwa tarehe 1 Septemba, 1964. Jeshi
letu liliadhimisha siku yao hiyo kwa kufanya zoezi kubwa la kivita
lililoanza Kibaha mkoani Pwani na kumalizikia Monduli Mkoani Arusha.
Nilibahatika
kushuhudia siku ya mwisho ya zoezi hilo. Nilifurahishwa sana na
kiwango cha utayari kivita cha Jeshi letu. Wanajeshi wetu walionesha
weledi wa hali ya juu, umahiri mkubwa, ujasiri, ukakamavu na
uvumilivu wa aina yake wakati wa kutekeleza majukumu yao katika
mazingira magumu ya uwanja wa medani za vita. Niliwapongeza siku ile
na narudia tena leo kuwapongeza. Niliyoyaona yamenihakikishia mimi na
Watanzania wote kuwa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
liko imara kulinda mipaka ya nchi yetu na kuhakikisha usalama wa
taifa letu na watu wake. Jeshi letu bado ni lile tunalolijua sisi
sote, lakini limezidi lile lililomng’oa mvamizi Dikteta Iddi Amin
wa Uganda, tena limezidi kwa mbali.
Mchakato
wa Katiba Mpya
Ndugu
Wananchi;
Mwaka
huu pia tumeshuhudia kukamilika kwa zoezi muhimu la kuandika Katiba
Inayopendekezwa. Kama tujuavyo sote, mchakato uliozaa Katiba
Inayopendekezwa ulikuwa na changamoto nyingi ndani na nje ya Bunge
Maalum la Katiba. Pamoja na hayo, Bunge hilo lilikamilisha kazi yake
kwa salama siku mbili kabla ya tarehe 4 Oktoba, 2014 ambayo ndiyo
ilikuwa siku ya mwisho. Mimi na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt.
Ali Mohamed Shein tulikabidhiwa nakala za Katiba Inayopendekezwa
tarehe 8 Oktoba, 2014. Nimeshatimiza wajibu wangu wa kuchapisha
katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni
kuwa tarehe 30 Aprili, 2015. Nimeshatoa maagizo kwa Tume ya Uchaguzi
kufanya matayarisho husika ya kuwezesha Kura ya Maoni kufanyika.
Ndugu
Wananchi;
Moja
ya mambo muhimu ambayo Tume ya Uchaguzi inafanya kwa sasa ni
kuandikisha wapiga kura katika Daftari la Mpiga Kura. Tume imeamua
kutumia mfumo mpya wa Biometric Voters Register. Uandikishaji wa
majaribio umefanyika katika baadhi ya Kata katika Majimbo ya Mlele,
Kawe na Kilombero. Matatizo yaliyojitokeza yatasaidia kuboresha
mfumo huo kabla ya uandikishaji wa watu wote wenye sifa stahiki
kuanza.
Ndugu
Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kuwafahamisha Watanzania wenzangu wote kuwa mfumo
mpya unatengeneza Daftari Jipya la Mpiga Kura ingawaje lugha
inayotumika ni uboreshaji wa Daftari la sasa. Uboreshaji huu wa
Daftari la Mpiga Kura ni tofauti na ule tuliouzoea ambapo walikuwa
wanaandikishwa wapiga kura wapya na wale waliopoteza vitambulisho
vyao. Safari hii wanaandikishwa wote wapya na wa zamani na wote
watapata vitambulisho vipya. Hivyo basi, sisi wenye vitambulisho vya
kupiga kura vya zamani tusifanye ajizi, tujitokeze kujiandikisha
wakati ukifika.
Jambo
la pili ni kwamba, Daftari la Mpiga Kura linalotayarishwa siyo kwa
ajili ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa peke yake, daftari
hilo hilo litatumika pia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Hivyo
basi, kujiandikisha ni jambo muhimu sana. Usipofanya hivyo siyo tu
utajinyima fursa ya kushiriki kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa
bali pia utakosa fursa ya kuchagua Rais wako, Mbunge wako na Diwani
wako. Katu usikubali yakukose hayo.
Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa
Ndugu
Wananchi;
Kama
mjuavyo tarehe 14 Desemba, 2014 na 20 Desemba, 2014 ulifanyika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuchagua viongozi wa vitongoji, vijiji
na mitaa. Uchaguzi umekwisha na viongozi wamekwishapatikana. Sasa ni
wajibu wa viongozi hao kufanya kazi waliyoiomba. Kwa walioendesha
uchaguzi ni wakati mzuri wa kufanya tathmini ili wapate mafunzo
yatokanayo na uchaguzi huo. Kwa TAMISEMI na Wakurugenzi Watendaji wa
Halmashauri, lengo liwe ni kuona namna ya kuimarisha mazuri na
kusahihisha makosa na matatizo yaliyojitokeza. Kwa walinzi wa amani
watambue matatizo ya kiusalama yaliyotokea na kuona namna ya
kutengeneza mikakati ya kuzuia matatizo ya namna hiyo yasijitokeze
tena. Hatma ya yote, shabaha yetu ni kutaka kufanya vizuri zaidi
katika chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa na kufanya vizuri zaidi
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Jumuiya
ya Afrika Mashariki
Ndugu
Wananchi;
Mwaka
huu Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Ni zamu yetu kwa mujibu wa mzunguko wa uongozi wa Jumuiya
yetu kati ya nchi wanachama. Ni dhamana kubwa na kwamba wenzetu wa
Afrika Mashariki wanatutegemea tuwaongoze katika kutekeleza malengo
na madhumuni ya Jumuiya kama yalivyoainishwa katika Mkataba
ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika,
tunategemewa kuongoza katika utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya
vikao vya Jumuiya. Hii inahusu maamuzi yaliyokwishafanywa kabla yetu
ambayo utekelezaji wake unaendelea na uamuzi mpya utakaofanywa katika
kipindi cha uongozi wetu.
Kwa
niaba ya Watanzania wote napenda kuwashukuru ndugu zetu wa Burundi,
Kenya, Rwanda na Uganda kwa kutuamini. Napenda kuahidi kuwa
hatutawaangusha. Sisi Watanzania tutafanya kila tuwezalo kuimarisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa manufaa ya Jumuiya yenyewe, nchi zetu
na wananchi wa Afrika Mashariki. Tutajitahidi kuwa wabunifu kwa nia
ya kuona utangamano unakua na kustawi kwa kasi na kuzaa matunda ya
maendeleo tunayoyatarajia sote. Matunda tuliyoyatarajia tulipoamua
kuanzisha Jumuiya hii na matunda tuliyoyapata tulipoamua kwa hiari
yetu kujiunga nayo kuwa wanachama.
SADC,
AU NA UN
Ndugu
Wananchi;
Kuhusu
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na
Umoja wa Mataifa, tunaahidi kuendelea kuwa wanachama waaminifu na
kushiriki kwa ukamilifu katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za
mashirika haya ya kikanda na kimataifa. Kwa upande wa SADC
tutaendelea kushiriki katika utekelezaji wa mikakati na mipango ya
maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ile ya kisiasa na kiusalama kama
ilivyoainishwa katika RISDP (Regional Indicative Strategic
Development Plan) na SIPO (SADC
Strategic Indicative Plan for the Organ). Kwa
ajili hiyo Tanzania, itaendelea kutoa mchango wake katika kukuza
utangamano wa kiuchumi katika SADC na kusaidia
kuimarisha uhusiano mwema na usalama miongoni mwa nchi wanachama wa
SADC. Hii ni pamoja na kusaidia katika kutatua migogoro ya kisiasa na
kusalama kati ya nchi wanachama.
Kwa
upande wa Umoja wa Afrika tutaendelea kutekeleza maamuzi ya vikao na
taasisi mbalimbali za Umoja huo. Daima tutakuwa wanachama waaminifu
wa Umoja wa Afrika na kuchangia katika uimarishaji wake. Kuhusu
Umoja wa Mataifa tutaendelea kutimiza wajibu wetu kama wanachama wa
Umoja huo wa kimataifa ulio adhimu na muhimu kwetu na dunia nzima.
Tutaendelea kushiriki katika shughuli za ulinzi wa amani chini ya
Umoja wa Mataifa. Hivi sasa tunao wanajeshi wetu katika majeshi ya
kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika nchi za Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo, Sudan na Lebanon. Tuko tayari wakati wote
kuchangia zaidi iwapo Umoja wa Mataifa watatutaka tufanye hivyo.
Hitimisho
Ndugu
Wananchi;
Namaliza
hotuba yangu hii ndefu kwa kuwashukuru Watanzania wote kwa kuiunga
mkono Serikali yetu na kwa mchango wenu uliowezesha nchi yetu kupata
mafanikio haya makubwa tunayojivunia katika mwaka 2014. Tumeweza
kuvuka mitihani na nyakati zenye majaribu mengi. Umoja wetu na
mshikamano wetu ndivyo vilivyotuwezesha kufika hapa. Tunauanza mwaka
2015 kwa matumaini makubwa. Mwaka 2015 unatupa fursa kubwa ya
kuendelea kuliimarisha zaidi taifa letu. Mwaka ujao ni mwaka wa
Uchaguzi Mkuu, hivyo huenda ukawa na changamoto na majaribu magumu
zaidi kuliko mwaka huu. Uelewa wetu, umoja wetu, mshikamano wetu na
moyo wetu wa uzalendo ndivyo vitakavyotuvusha kama ilivyokuwa kwa
miaka ya nyuma. Mimi nina imani kubwa kwa uwezo na utayari wa
Watanzania wenzangu kuidumisha sifa nzuri ya nchi yetu ya umoja na
mshikamano wa watu wake uliozaa amani na utulivu. Tumeweza mwaka huu
na miaka ya nyuma, tutaweza tena mwakani na miaka ijayo. Inawezekana,
Timiza Wajibu Wako! Nawatakia heri ya mwaka mpya.
Mungu
Ibariki Afrika!
Mungu
Ibariki Tanzania!
Asanteni
kwa kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment