Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) mkoani Geita, kimepata pigo baada ya mshindi wa
nafasi ya ujumbe wa viti maalum katika uchaguzi uliofanyika jana
Jumapili katika mtaa wa Msalala Geita mjini, Bertha Chimani miaka 32,
kukutwa katika shimo la choo lisilotumika akiwa amefariki dunia.
Chimani ambaye alipata
kura nyingi katika uchaguzi huo, aliwaaga wenzake waliokuwa
wakisubiri kushangilia ushindi huo akiwamo dada yake kuwa anakwenda
kujisaidia lakini hakuweza hakurejea mpaka mwili wake ulipogundulika
jana asubuhi.
Mwili wake ulikutwa
ukielea katika shimo la choo kilichokuwa hakijafunikwa ndani ya uzio
wa jengo lililokuwa linatumika kwa ajili ya kupigia na kuhesabia kura
lenye urefu wa zaidi ya futi 30.
Kamanda wa polisi mkoa wa
Geita, Joseph Konyo, amethibitisha kutokea tukio hilo na kudai
marehemu alitumbukia katika shimo hilo usiku na mwili wake uliopolewa
na kikosi cha zimamoto na kuhifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti cha
hospitali ya wilaya ya Geita kwa uchunguzi zaidi.
Katika tukio lingine
lililotokea leo, Simeo Isaka miaka 42, mkazi wa kijiji cha Ngokolo
kata ya Bukomela tarafa ya Mweli wilayani Kahama, ameuawa kwa kukatwa
na jembe kichwani wakati akishangilia matokeo ya ushindi wa chama
chake cha Chadema.
Kamanda wa Polisi mkoani
Shinyanga, Justus Kamugisha, amesema tukio hilo limetokea usiku wa
kuamkia leo wakati Isaka akishangilia matokeo ya uchaguzi wa serikali
za mitaa wa kijiji cha Ngokolo.
0 comments:
Post a Comment