Mkuu wa wilaya ya siha Dk. Charles Mlingwa
Migogoro baina ya wafugaji na
wawekezaji katika maeneo mbalimbali nchini, imeanza kuleta athari za
kijamii na kiuchumi, baada ya taasisi za kielimu huko West
Kilimanjaro, kulalamikia hatua ya usitishwaji wa huduma ya chakula
mashuleni, pamoja na wasambazaji wa mazao kukosa soko kutokana na
migogoro hiyo.
Kituo hiki kimelazimika kufuatilia moja
ya mkasa uliojiri mwezi Novemba 2014 katika Ranchi ya Ndarakwai
iliyopo Wilaya ya Siha Magharibi mwa Kilimanjaro ambapo athari za
migogoro hiyo zinajionyesha wazi
Novemba 14 mwaka huu Kambi iliyopo
ndani ya Ranchi ya Ndarakwai iligeuka majivu matupu pamoja na mali
zingine kuharibiwa vibaya baada ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafugaji
kutekeleza mpango huu kwa madai ya kugombea malisho.
Uongozi wa Wilaya ya Siha kupitia kwa
Mkuu wake wa Wilaya Dr.Charles Mlingwa unalitafsiri tukio hili kuwa
la kihalifu ambalo limejiri baada mifugo ya vijiji vinavyozunguka
Ranchi hiyo pamoja na maeneo ya Longido kuingizwa ndani ya Ranchi na
baadaye askari kulazimika kuitoa kitendo kilichozua tafrani na
baadaye wafugaji kulipiza kisasa kwa kuteketeza kambi ya mwekezaji.
Kituo hiki kimeangazia namna athari za
mgogoro huu zinavyozikumba sekta zingine ambapo pia uongozi wa Ranchi
umeeleza kusitisha mikataba ya wafanyakazi wake zaidi ya70 kutokana
na janga hilo.
Shule ya Msingi Olmolok yenye wanafunzi
mia nne ambayo ilikuwa ikinufaika na mpango wa chakula shuleni
kutokana na uwekezaji katika Ranchi ya Ndarakwai sasa mpango huo
umesitishwa na Mwalimu Mkuu wake msaidizi Betwel Mwasha anasema
mahudhurio na kiwango cha taaluma vimeporomoka kwa kasi.
Mfanyabiashara wa Nyama katika kijiji
cha Ngarenairobi Samwel Lizer aliyekuwa akisambaza kitoweo hicho kwa
wanafunzi wa Shule ya Vetenari anasema mapato aliyokuwa akikusanya
kwa kusambaza kilo 40 kila mwezi sasa yamesitishwa na hivyo
kumsababishia hasara.
Katika Kijiji cha Miti Mirefu mfugaji
mmoja wa kuku mama Julieta Baltazari aliyengia mkataba wa kusambaza
mayai amebainisha kuathiriwa na mgogoro huo baada ya kusitishwa kwa
mkataba.
Mkurugenzi Mkuuu wa Ranchi ya Ndarakwai
Peter Jones anasema wameaua kusitisha huduma zote za kijamii kwa sasa
kutokana na hasara iliyotokea baada ya nyumba ishrini ,magari sita
pamoja na mali zingine zilizokuwa katika kambi yake kuteketezwa kwa
moto na hivyo kufanya hasara inayofikia dola milioni moja..
Uwekezaji wa kipindi cha miaka 19
unaoendena na biashara ya utalii wa upigaji picha katika eneo hili
lililo umbali wa kilometa 50 tokea katika hifadhi ya wanyama ya
Amboseli nchini Kenya huwenda ukatoweka iwapo hakutakuwepo kwa hatua
za dharura kumaliza mgogoro huu ambao ni taswira ya kile kinachojiri
katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
0 comments:
Post a Comment