Mara baada ya kuundwa kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya
CCM Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu Ndg. Abdulrahman Kinana mwanzoni mwaka
mwaka jana, Sekretarieti hiyo imejiwekea utaratibu wa kufanya ziara mikoani
kukutana na wananchi kusikiliza kero zao,kukagua utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM na kuimarisha Chama mikoani. Utaratibu huu ni agizo la mkutano
mkuu wa Taifa wa nane wa CCM uliofanyika Novemba 2012 mjini Dodoma. Nanukuu
azimio hilo;
“ Chama Cha Mapinduzi lazima kiwe karibu na wananchi,
kisikilize changamoto zao na kiwasemee wananchi na hasa wanyonge” Moja ya maazimio
ya Mkutano Mkuu wa nane wa CCM 2012.
Kwa hiyo msingi wa kwanza wa ziara hizo ni maagizo ya
Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambacho ndicho kikao cha juu kabisa cha Chama. Msingi
wa pili ni ukweli kuwa CCM ndio iliyopewa dhamana na kuingia mkataba na wananchi
kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015, hivyo inayowajibu wa
kukagua utekelezaji wa ilani hiyo.
Na bila shaka wote tumeshuhudia jinsi ziara hizo zilivyoinua
uhai wa Chama nchi nzima na kuongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
na kutatua kero mbalimbali za wananchi kwenye maeneo yao, kiasi cha kuongeza
imani ya wananchi kwa CCM.
Tumeshuhudia makundi mbalimbali ndani ya jamii yakija
kueleza changamoto zao ndani ya Chama. Makundi hayo ni pamoja na makundi ya
wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wanafunzi na wafanyakazi hasa walimu. Huu
ni uthibitisho wa kuongezeka kwa imani yao kwa CCM.
Katika mwendelezo wa ziara hizo mwishoni mwa mwaka jana
Katibu Mkuu wa CCM na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti walifanya ziara ya siku
26 katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe. Pamoja na mambo mengine wananchi
walilalamikia baadhi ya watendaji wa serikali hasa baadhi ya mawaziri wakiamini
kuwa yapo mapungufu kadhaa yanayotokea kwenye wizara zao.
Naomba upokee tamko hili kutoka kwa katibu wa itikadi na
uenezi ndugu Nape Nnauye, alilolitoa leo majira ya saa nne, makao makuu ya
chama cha mapinduzi CCM jijini dar es salaam mbele ya waandishi wa habari.
NB: komputer yangu adobe inasumbua so natuma sauti, utaandaa
hii habari ni nzuri sana kwetu.
Tamko
CCM kama lilivyo agizo la Mkutano mkuu la kuwasemea wananchi
tulisikiliza kilio chao na kwa kufuata utaratibu, baadhi ya mawaziri hao
waliitwa na kuhojiwa kwenye Kamati Kuu ya CCM mwezi Disemba 2013.
Utaratibu wa
watendaji wa serikali kutoa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
kwenye vikao vya Chama sio mgeni na wala haujaanza jana. Wakuu wa wilaya hutoa
kwenye wilaya, wakuu wa mikoa hutoa mikoani kwao,hivyo sio utaratibu mpya.
Baada ya mahojiano hayo Kamati Kuu ya CCM ilitoa ushauri kwa
serikali wa namna ya kurekebisha mapungufu yaliyoelezwa na wananchi. Kwakuwa
kwa mujibu wa Katiba ya Nchi mwenye mamlaka na mawaziri ni Rais mwenyewe, CCM
ililiacha suala hili kwake aangalie njia ipi bora ya kuondoa mapungufu
tuliyoyaeleza.
Na kwenye taarifa yetu kwa vyombo vya habari baada ya kikao
hicho tulisisitiza kuwa sio lazima awafukuze mawaziri husika isipokuwa wanaweza
kufanya mabadiliko katika mfumo,sheria nk ili mradi kuwepo na mabadiliko katika
kushughulikia mambo yaliyolalamikiwa na wananchi.
Hivi karibuni Rais amefanya mabadiliko kidogo kwenye baraza
lake la mawaziri na kuwarudisha baadhi ya mawaziri waliolalamikiwa na wananchi
na wabunge, ambao malalamiko hayo yaliungwa mkono na CCM. Ni kupitia malalamiko
hayo ndipo lilipozaliwa jina la mawaziri mizigo. Baada ya uteuzi huo kukaibuka
mjadala mkubwa nchini wakihoji kulikoni Rais kaamua kutowatimua mawaziri hao.
Kwanza haikua hoja ya CCM kuwafukuza mawaziri hao bali
kuchukua hatua za kurekebisha mapungufu husika. Kufukuza inaweza kuwa ni njia
ya kutatua tatizo lakini sio njia pekee. Hivyo basi CCM tunaamini kuwa
kurudishwa kwao wamepewa fursa ya kurekebisha mapungufu tuliyoyasema kwa niaba
ya wananchi. Tunaamini mawaziri wote hawatabweteka bali watatimiza wajibu wao
na kuhakikisha wanawatumikia wananchi ambao ndio waajiri wa serikali.
Ifahamike kuwa Chama Cha Mapinduzi hakitasita kuchukua hatua
kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha
mapungufu na watakaoshindwa kutimiza wajibu wao vizuri. Wakumbuke kushindwa
kwao kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa Ilani ya uchaguzi ya CCM, CCM
haitavumilia usaliti huo. Kukaa kimya kwa CCM itakua ni kujinyonga yenyewe
jambo ambalo hatutaruhusu kabisa.
Tunajua wapo baadhi ya watendaji wa serikali wasiopenda
kuhojiwa utendaji wao, tunawasihi kwa moyo safi wasiotaka kuulizwa juu ya
utendaji wao waondoke serikalini wenyewe kwani CCM tutakuwa wakali sana kwenye
mapungufu,kwani tukikaa kimya tutakua tunajihujumu wenyewe.
Tutatumia vizuri wingi wa wabunge wetu bungeni na wingi wa
madiwani wetu kwenye halmashauri kuisimamia vizuri serikali. Hivyo kuanzia sasa
kasi ya CCM kuisimamia serikali, kuisifu itakapofanya vizuri na kukosoa
itakapofanya vibaya itaongezeka mara dufu kwa kila ngazi.
Tunawaomba watanzania kwa ujumla tuwape muda wateule hawa wa
Rais watimize wajibu wao, lakini tusisite kusema pale tutakapoona mambo
hayaendi kama tunavyotarajia. Uwajibikaji wa kweli ndio msingi wa mafanikio na
maendeleo yetu.
CCM inawatakia kila lakheri kwenye kutimiza wajibu wao. Tuna
matumaini makubwa kuwa wote kwa pamoja hawataisaliti ilani ya Uchaguzi ya CCM
na kwamba hawatayaangusha matumaini ya wananchi kwa serikali yao.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
MWISHO
0 comments:
Post a Comment